Nahodha wa zamani wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' amezitabiria Simba na Yanga katika mechi zao za robo fainali zinazochezwa leo na kesho akisema zina nafasi ya kutinga nusu fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika, ila akiwataka wachezaji wajiamini na wafunge mabao mengi Kwa Mkapa.
Leo Ijumaa, Simba inacheza dhidi ya Al Ahly katika mechi itakayopigwa kuanzia saa 3:00 usiku na Cannavaro anaona ushindi upo wazi kwa Wanamsimbazi, akiwasisitiza wachezaji wafunge mabao mengi kwa kadri watakavyoweza ili presha iwe kwa wapinzani wao.
2016 Yanga ikiwa chini ya kocha Hans van der Pluijm, Cannavaro aliipa ushindi wa bao 1-0 timu yake, akifunga bao la kichwa, mechi ya marudiano kule Masri ilimalizika kwa sare ya bao 1-1, Cannavaro amesema hakuna mtu aliyetegemea matokeo hayo, ila iliwezekana.
"Simba ina uwezo wa kuifunga Al Alhy zaidi ya bao moja, ili ikienda mechi ya marudiano itawafanya wajiamini na mpinzani acheze kwa presha inayoweza ikawapa ushindi ugenini," amesena na kuongeza;
"Mbali na matokeo ambayo Yanga tulipata kwa Al Ahly, kuna mechi nyingi za kimataifa, hatukufanya vizuri nyumbani, tukashinda ugenini, hivyo hakuna linaloshindikana, wazingatie nidhamu, kujiamini na kutumia nafasi."
Aliuzungumzia mchezo wa Yanga dhidi ya Mamelodi Sundowns utakaopigwa kesho Jumamosi nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania amesema; "Wachezaji wa Yanga kila mmoja wao, ajitoe kizalendo kwa timu yake, ushindi unawezekana. Kama Yanga ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka jana, ikicheza dhidi ya USM Alger sioni kinachoweza kikaikwamisha, kwani tayari timu zetu zina hatua kubwa ya ushindani."
Simba na Yanga zilizifika hatua hiyo ya robo kwa kumaliza nafasi ya pili katika makundi ya B na D yaliyoongozwa na Asec Mimosas ya Ivory na Al Ahly.
SIMBA VS AL AHLY 2023 (AFL) Simba 2-2 Al Ahly Al Ahly 1-1 Simba
2020-2021-CAFCL Simba 1-0 Al Ahly Al Ahly 1-0 Simba
2018-2019 (CAFCL) Simba 1-0 Al Alhy Al Ahly 5-0 Simba.
1985 (Washindi) Simba 2-1 Al Ahly Al Ahly 2-0 Simba