Benchikha: Tulieni, ngoma haijaisha!

 

Benchikha: Tulieni, ngoma haijaisha!

Simba imepoteza kwa mara ya kwanza nyumbani mbele ya Al Ahly ya Misri kwa kufungwa bao 1-0 katika pambano la kwanza la robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha amewatuliza wachezaji na mashabiki akisema mechi haijaisha hadi iishe Cairo.


Kipigo hicho ni cha kwanza kwa Simba tangu ianze kukutana na Al Ahly katika mechi za CAF kuanzia mwaka 1985, kimeonekana kuitengenezea ugumu Wekundu hao kwenye harakati za kutaka kutinga nusu fainali kwa sasa inalazimika kwenda kulipa kisasi Cairo kwa ushindi zaidi ya bao moja ili isonge mbele.


Hata hivyo, rekodi zinaonyesha Simba haijawahi kupata ushindi ugenini mbele ya Al Ahly, kwani mechi nne zilizopita ikiwamo moja ya Kombe la Washindi 1985 na mbili za makundi ya Ligi ya Mabingwa zimefungwa zote na moja ya michuano mipya ya African Football League imeishia kwa sare ya 1-1.


Ile ya mwaka 1985 ililala 2-0, moja ya makundi msimu wa 2019 ilipigwa 5-0, kisha ikalala 1-0 mwaka 2021 na katika AFL iliyopigwa Oktoba mwaka jana ilitoka sare ya 1-1.


Licha ya kuonekana Simba ina mlima mrefu kutokana na ubora wa vikosi na hata mchezaji mmoja mmoja kulinganisha na wale wa Al Ahly, kocha Benchikha aliyeifunga timu hiyo ya Misri bao 1-0 katika mechi ya CAF Super Cup akiwa na USM Alger ya Algeria kabla ya kuja Msimbazi, ametamba haamini kama mechi baina yao na Wamisri ndo imeishia kwa Mkapa.


Benchikha alisema anaamini Simba ina nafasi ya kupindua meza ugenini hata kama inaonekana ni ngumu, kwa kutaka kufanyia kazi dosari zote zilizoiangusha timu kwenye mchezo wa juzi ambapo kosa moja la safu ya ulinzi iliwapa faida Al Ahly kutibua rekodi ya mnyama kwenye uwanja wa nyumbani.


Kocha huyo, aliliambia Mwanaspoti mechi haijaisha na kama wenzao walishinda ugenini basi hata wao wana nafasi ya kusahihisha makosa na kupata ushindi kwani soka lina matokeo ya kushangaza na huwa haijalishi timu zinacheza uwanja gani, ilimradi zimejiandaa vya kutosha na kupambana kwa dakika zote.


MSIKIE MWENYEWE


Benchikha alisema licha ya kikosi hicho kushindwa kupata matokeo mzuri juzi usiku, lakini timu ilicheza vema na kilichowaangusha ni kutotumia nafasi nyingi ilizozitengeneza ambazo kama mastaa wa timu hiyo wangekuwa na utulivu ingetoka na ushindi mnono nyumbani mbele ya watetezi hao wa taji.


Pia alisema licha ya kutopata ushindi, lakini amefurahisiwa na namna kiungo Fabrice Ngoma alivyocheza na kwake ndiye aliyekuwa nyota wa mchezo wa Simba na aliangushwa tu kwa kukosa mizani nzuri na wenzake.


"Malengo ni yale yale ya Simba kwenda nusu fainali, ni kweli tumepoteza kutokana na makosa yetu wenyewe. Washambuliaji walikosa umakini kutupia mipira nyavuni. Tunaenda kuzungumza na wachezaji hao na kurekebisha kila kitu ili tupate matokeo mazuri ugenini," alisema Benchukha aliyekiri Willy Onana ni mchezaji mzuri, ila bado hajarudi kwenye ubora tangu alipotoka majeruhi.


"Niwaombe radhi mashabiki ambao wamekuwa sehemu ya mafanikio ya Simba kwa kujitokeza na kuiunga mkono timu, tunajua wameumia kwa matokeo haya, lakini bado tuna nafasi ya kurekebisha kwa dakika 90 zilizosalia za ugeninim," alisema Benchika na kuongeza;


"Nitazungumza na wachezaji na kuwaambia wasikate tamaa na matokeo haya, tujipange na kwenda Cairo tukiwa na dhamira moja ya kuleta furaha kwa mashabiki kwani nafasi hiyo ipo. Ni kweli Al Ahly ni timu kubwa na ina kikosi bora, lakini inafugika."


REKODI ZILIVYO


Hata hivyo, rekodi ya Al Ahly ikiwa nyumbani ni nzuri kwani haijapoteza mchezo wowote tangu Mei mwaka jana katika michuano yote, ukiondoa kipigo cha 1-0 kutoka kwa USM Alger katika mechi ya CAF Super Cup ambao wao walikuwa wenyeji ila ikichezwa Uwanja wa usio na mwenyewe.


Mechi hiyo ilipigwa Septemba 15 mwaka jana kwenye Uwanja wa Kimataifa wa King Fahd uliopo Riyadh, Saudi Arabia, lakini kwa michezo wa kimataifa, ya ligi na vikombe vya ndani tangu Mei, 2023 timu hiyo haijapoteza zaidi ya kushinda 19 na kupata sare tano, jambo linaloipa kibarua kizito Simba.


Mechi ya marudiano ya Al Ahly na Simba itapigwa Ijumaa ijayo jijini Cairo kuanzia saa 5:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na mshindi wa jumla atatinga nusu fainali kuumana na mshindi wa robo fainali nyingine kati ya Esperance ya Tunisia na Asec Mimosas ya Ivory Coast zilizokuwa zikicheza jana usiku.


Mara ya mwisho kwa Simba kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ilikuwa ni mwaka 1974 enzi michuano ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika ikifungwa na Mehalla El Kubra ya Misri kwa penalti 3-0 baada ya kila moja kushinda mchezo wa nyumbani kwa bao 1-0.


Pia Simba haina rekodi nzuri kwa mechi za ugenini za kimataifa, kwani kwa msimu huu pekee katika mechi nne ilizocheza hadi kufika robo fainali, haikushinda hata moja zaidi ya kufungwa na Wydad CA ya Morocco bao 1-0, kisha kutoka sare michezo mingine mitatu ikiwamo dhidi ya Power Dynamos ya Zambia (2-2), Jwaneng Galaxy ya Botswana (0-0) na Asec Mimosas (0-0).


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad