Aucho alikuwa nje ya uwanja kwa majeraha tangu alipoumia kwenye mechi ya mwisho hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly na kufanyiwa upasuaji mdogo wa goti na kumfanya akose mechi nne za Ligi Kuu Bara ya Namungo, Geita Gold, Ihefu naAzam FC.
Mchezaji huyo amekuwa nguzo imara kwa safu ya ulinzi na kiungo ya Yanga kwa aina ya uchezaji wake na kukosekana kwake kwenye mechi hizo nne pengo lake lilizibwa na wachezaji wawili tofauti, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Dickson Job ambaye ni beki wa kati.
Katika mechi hizo, Yanga ilishinda michezo mitatu, lakini ikapasuka 2-1 kwa Azam na kulikuwa na hofu Aucho atakosekana katika mechi za robo fainali dhidi ya Masandawana kutoka Afrika Kusini.
Hata hivyo, kwa sasa nyota huyo wa kimataifa wa Uganda, tayari ameanza mazoezi na wenzake tangu Jumatatu baada ya kufuzu vipimo vya uponaji wa jeraha alililokuwa nalo na ana matumaini ya kucheza mechi ya kwanza ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns Jumamosi hii.
Galiwango aliyekuwa na katika kikosi cha ‘The Cranes’ sambamba na Aucho kilichoshiriki michuano ya Afcon 2019 zilizofanyika Misri, alisema kiungo huyo mkongwe ameendelea kuwa bora na mfano kwa wenzake kutokana na nidhamu na kucheza kwa kujituma muda wote.
Beki huyo wa kushoto wa Kagera, alisema Aucho amekuwa mfano wa kuigwa kwa jinsi anavyopambana kuonyesha uwezo na ubora wake uwanjani hadi kuwa chachu kwa wachezaji chipukizi.
“Nimejifunza mengi kutoka kwake, nafikiri kinachombeba na kumfanya awe bora ni kuzingatia mazoezi na nidhamu ya ndani na nje uwanja kwa namna anavyoishi anatupa hamasa hata sisi,” alisema beki huyo, huku shabiki wa Yanga jijini hapa, Victor Ndulu alisema kukosekana kwa Khalid Aucho katika safu ya kiungo kumeipa pengo timu hiyo na kurejea kwake kunaongeza matumaini.
Yanga inatarajiwa kuwa uwanjani Jumamosi kuikabili Mamelodi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa mechi itakayoanza saa 3:00 usiku kabla ya kurudiana Aprili mjini Pretoria na mshindi wa jumla atafuzu kwenda nusu fainali ya michuano hiyo.
Mshindi wa mechi hiyo atapata nafasi ya kucheza na Esperance ya Tunisia au Asec Mimosas ya Ivory Coast zitakazoumana nazo katika mechi nyingine ya robo fainali wikiendi hii, huku Yanga ikiwa na deni la kulipa kisasi cha kung’olewa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2001.
Katika mechi hizo mbili za mwaka 2001, Yanga ilichapwa 3-2 ugenini kisha ikatoka sare ya 3-3 na kutolewa kwa jumla ya mabao 6-5.