5G za Yanga SC zaitisha timu Ligi Kuu

5G za Yanga SC zaitisha timu Ligi Kuu


Dodoma Jiji inaendelea kujifua kujiandaa na mechi ya hatua ya 16 Bora za Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Yanga, huku benchi la ufundi likiwakomalia mabeki ili kuepuka aibu ya kupigwa 5-0 kama timu nyingine zilizokutana na wababe hao katika michuano hiyo na Ligi Kuu.


Yanga imegawa dozi ya 5G kwa timu tisa msimu huu ikiwamo Simba iliyolala 5-1, huku katika ASFC imezipiga timu zote ilizocheza nazo hadi kufika 16 Bora.


Ilianza kwa kuifumua Hausung ya Njombe kwa 5-1 kabla ya kuipasua Polisi Tanzania 5-0 na kufika 16 Bora ikitarajiwa kukutana na Dodoma Aprili 10 mjini Dodoma na wenyeji wamejishtukia na kuanza kujipanga kuimarisha safu ya ulinzi iliyoruhusu mabao mengi katika Ligi Kuu hadi sasa.


Dodoma katika mechi 20 ilizocheza ikishika nafasi ya 10 kwa pointi 23 imeruhusu mabao 21 jambo lililoLifanya benchi kurejea kambini mapema na kuikomalia safu hiyo iepuke aibu ya 5G.


Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Kassim Liogope alisema baada ya kurejea kambini wameridhishwa na afya za wachezaji na kwamba hesabu zao zipo kwa Yanga na mabao 21 waliyofungwa katika ligi yamewazindua kujipanga kabla ya kukutana na watetezi hao.


Liogope alisema aibu ya hivi karibuni kupigwa 4-1 na Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex bado inawasumbua na hawataki nyingine kutoka kwa Yanga.


“Pia hata mabao ya kufunga si mengi sana kama tunavyotaka, hivyo tunaisuka timu ili kabla ya mchezo dhidi ya Yanga tuwe imara idara zote, tumeipa zaidi jicho beki kutokana kuruhusu mabao mengi na Yanga huwa inafanyia sifa ikikutana na timu legelege,” alisema Liogope, huku beki wa timu hiyo, Abubakar Ngalema akisema wapo makini kufuata na kutekeleza maelekezo ya makocha ili kuepuka makosa yasijirudie.


Ngalema alisema hata matokeo iliyonayo Dodoma Jiji bado sio mazuri mbele ya Yanga, lakini kiu ni kuona timu inasonga mbele hatua ya robo fainali ndio maana wamekuwa makini mazoezini.


Timu nyingine zilizokumbana na vipigo vya 5G kutoka kwa Yanga ni JKT Tanzania, KMC na Ihefu zilizofungwa 5-0 katika Ligi Kuu Bara, huku Jamhuri ilifumuliwa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi na Asas ya Djibouti ilipasuka 5-1 katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa.


Michuano ya 16 Bora ya ASFC inatarajiwa kuanza kupigwa Aprili 02 kwa Namungo kuumana na Kagera Sugar, kabkla ya siku inayofuata Geita Gold kucheza na Rhino Rangers na April 4 itakuwa zamu ya Singida FG dhidi ya Tabora United, kisha Coastal Union na JKT Tanzania kuumana siku inayofuata.


Mechi nyingine za hatua hiyo ni kati ya KMC dhidi ya Ihefu itakayopigwa Aprili 6 na siku inayofuata itakuwa zamu ya mabingwa wa zamani wa taji hilo, Azam na Mtibwa Sugar zitaonyeshana kazi na Aprili 9 kazi itahamia Kigoma kwa Mashujaa FC kuialika Simba, ndipo Yanga na Dodoma zitafungia pazia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.