Yanga Wameshamsahau Kimoja FISTON Mayele na Majini yake, Kocha Gamondi Afanya Kazi Kubwa Kuziba Pengo



KABLA hajapanda ndege kwenda Riyadh, Saudi Arabia, msimu mmoja nyuma yake Manchester City walikuwa mabingwa wa Ligi Kuu England na mfungaji bora alikuwa Riyad Mahrez. Alifunga mabao 24 ya msimu katika ligi hiyo. Ulikuwa msimu wake bora zaidi England.


Hivi ndivyo ambavyo Yanga wameziba pengo la Fiston Mayele mpaka sasa? Inawezekana. Tusubiri mpaka mwisho wa msimu, lakini mpaka sasa ndivyo ambavyo inaonyesha. Yanga wanajaribu kufanya kile ambacho Pep Guardiola amewahi kukifanya katika soka.


Guardiola ni muumini wa kutengeneza nafasi katika soka halafu mchezaji yeyote anafunga. Aliwahi kufanya hivyo akiwa na Barcelona. Kuna nyakati alikuwa anaichezesha Barcelona bila mshambuliaji. Angeweza kumuweka nje David Villa na nafasi yake ingekwenda kwa Lionel Messi. Yeyote katika kiungo au mawinga angeweza kufunga.


Labda ni namna ambavyo Yanga wameziba pengo la Mayele bila kujua. Mabao hayajaenda sana kwa Kennedy Musonda wala Clement Mzize. Mabao ambayo Mayele alikuwa anafunga yamekwenda zaidi kwa wachezaji wa viungo. Mpaka sasa kinara wa mabao ni Aziz Ki ana mabao 10.



Mabao ya Aziz ambaye ni kiungo yasingetosha kuiweka Yanga kileleni. Maxi Nzingeli ana mabao manane wakati Pacome Zouzoua ana mabao sita, huku Mudathir Yahya akiwa na mabao sita. Kwa ujumla mpaka sasa viungo hao wa Yanga wana mabao 30.


Wakati huohuo mpaka kufikia hatua hii Mayele alikuwa na mabao 10 ingawa mpaka mwishoni mwa msimu alifunga mabao 17. Ina maana mpaka sasa viungo wapya wawili wa Yanga, Pacome na Maxi wameshafunga mabao ambayo Mayele alikuwa amefunga mpaka hatua hii ya ligi. Wamefunga kwa jumla mabao 12.


Wamebakisha mabao matano tu kufikia mabao ambayo Mayele alifunga msimu mzima katika ligi. Ni jambo linalowezekana kama tu Yanga wakiendelea kutengeneza nafasi kama ambavyo wamekuwa wakifanya. Hii ndio ambayo ilikuwa falsafa ya Guardiola. Ukitengeneza nafasi basi yeyote anaweza kufunga.

Ukiachana na Pacome na Maxi ambao ni wapya, viungo wawili wa zamani Mudathir na Aziz wamekuwa na hamu ya kufunga. Aziz ambaye msimu uliopita alikuwa na msimu mbovu tayari amefunga mabao 10 na anaongoza kwa kufunga mabao katika Ligi Kuu. Hii imewasaidia kuziba nafasi ya Mayele.


Wengi walitazamia Yanga izibe pengo la Mayele kwa kumpata mshanbuliaji ambaye atafunga mabao 20. Siku hizi kuna mambo mawili yametokea katika soka. Kwanza ni viungo kufunga sana kwa mujibu wa mifumo ya soka. Hizi ndizo nyakati ambazo unaambiwa kuwa wakati mwingine sio lazima mshambuliaji afunge sana, bali anaweza kuwa na sifa ya kutengeneza nafasi kwa wengine.


Katika Kombe la Dunia mwaka 2018 pale Russia, Ufaransa walitwaa bila mshambuliaji wao, Olivier Giroud kufunga bao. Kocha Didier Deschamps aliamini kwamba Giroud alikuwa bora zaidi uwanjani kwa kuwatengenezea nafasi wenzake. Ni kitu kigumu kuingia katika akili ya shabiki wa zamani. Kwa sasa dunia imebadilika.


Lakini pia dunia yenyewe nayo imebadilika. Siku hizi kuziba pengo la mshambuliaji imekuwa habari ngumu. Kama unaweza kumpata mshambuliaji atakayefunga mabao 17 kama Mayele, basi una bahati. Akikuponyoka unaweza usimpate mshambuliaji wa namna hiyo kiurahisi.


Hii sio kwa Yanga tu, bali kwa dunia nzima. Washambuliaji wamekuwa wachache. Haishangazi kuona kwamba ilikuwa wazi Yanga wangempoteza Mayele baada ya msimu ule mzuri wa ligi na michuano ya Kombe la Shirikisho. Lazima wakubwa walikuwa wanamtamani.


Nilijua kwamba Yanga wangepata shida kupata mbadala wa Mayele. Ni kama ambavyo Mamelodi Sundowns watapata shida kupata mbadala wa Peter Shalulile. Wafungaji ni haba Afrika. Wafungaji ni haba duniani kwa ujumla. Unaweza kusaidiwa kwa kugawanya mabao kwa wachezaji wako. Fikiria kwamba kwa Yanga hata Dickson Job na Yao Kouassi wamefunga katika ligi.


Kitu kingine ambacho labda kilikuwa kikwazo kwa Yanga kutawanya mabao yao ni uwepo wa Mayele. Ukiwa na mshambuliaji kama yeye timu nzima inamuangalia katika ‘muvu’ zake. Ni jambo la kawaida tu. Unapokuwa na mchezaji kama yeye ghafla kila mchezaji anamuona kwamba ndiye mchezaji anayepaswa kupelekewa mpira wa mwisho (focal point).


Anapokosekana mchezaji wa aina yake, basi huduma za mwisho zinatawanywa kwa wachezaji tofauti wanaochukua nafasi. Pambano la juzi (dhidi ya KMC), Nickson Kibabage alimtazama Mudathir katika nafasi akampasia, akafunga. Ilipotokea nafasi nyingine akamtazama Pacome akiwa katika nafasi akampasia, akafunga. Mimu uliopita labda angemtazama zaidi Mayele yupo wapi. Matokeo yake Yanga inaweza kuchukua ubingwa bila kuwa na mshambuliaji mwenye mabao 10. Kama wakiendeleza tabia hii wanaweza kuwa na mfungaji bora ambaye ni kiungo. Ni kilekile kilichowatokea City kwa Mahrez. Lakini Liverpool hii iliyotamba na inayoendelea kutamba mfungaji wao bora siku zote amekuwa Mo Salah.


Ndio maana labda bila ya Mayele msimu huu kufikia hatua hii Yanga wamefunga mabao 39 wakati wakiwa na Mayele walikuwa wamefunga mabao 27. Papo hapo kufikia hatua hii walikuwa wana pointi 40, lakini kwa sasa wanazo 43. Huu ni mwendelezo mkubwa tangu Mayele alipoondoka ingawa kwa kawaida hofu inabaki palepale kwamba Yanga wanapaswa kuziba pengo la Mayele.


Lakini papo hapo kuna jambo la kujiuliza kuhusu ubora wa kocha aliyepita, Nasireddine Nabi na kocha wa sasa Manuel Gamondi. Ngumu kujua tofauti yao kwa namna Yanga inavyocheza. Kuna watu wamekuwa na wasiwasi na Gamondi baada ya hivi karibuni Yanga kusuasua katika ufungaji.

Hata hivyo ukifuatilia namba unaweza kuona kuwa Gamondi anaweza kuwa bora kuliko Nabi mpaka sasa. Tunapaswa kusubiri na kuona mpaka mwishoni nani ataibuka mbabe.


Kuanzia uzibaji wa pengo la Mayele hadi namna ambavyo Nabi na Gamondi wanaweza kutofautiana katika ubora. Niandikie maoni yako: 0658 376 417

Mwanasporti

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad