Matola, Benchikha wagawana usajili Simba

Matola, Benchikha wagawana usajili Simba


Kocha mpya wa Simba, Abdelhak Benchikha, raia wa Algeria ambaye alitua na msaidizi wake Farid Zemiti na kocha wa viungo Kamal Boudjenane amempa mzawa, Seleman Matola jukumu la kupendekeza na kusajili wachezaji wazawa kwenye dirisha hili la Januari.


Matola ambaye ana mkataba wa kuifundisha timu ya vijana ya Simba alirudishwa timu kubwa baada ya kuondolewa kwa kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ hivyo uongozi wa Simba ulimpa nafasi hiyo Matola na Daniel Cadena kukaimu hadi walipompata kocha mpya.


Habari za ndani ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Benchikha ameridhia kumpa jukumu hilo Matola ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba, kwani anawajua vizuri wachezaji wa ndani zaidi yake na Bodi ya Wakurugenzi ya Simba pia imebariki suala hilo.


Chanzo cha kuaminika cha Mwanaspoti kimesema kwenye usajili Matola atashirikiana na Cadena kuandaa ripoti nzima ya kikosi chao na kutoa mapendekezo ya nani abaki na nani waachane nao katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo unaofunguliwa rasmi Desemba 16, mwaka huu.


Mwanaspoti linajua kwamba baada ya usajili kukamilika basi uwepo wa Matola kwenye kikosi hicho utaamuliwa na Benchikha ambaye kama ataendelea kumuhitaji atabaki lakini kama ataona imetosha basi Matola atarudi kwenye majukumu yake ya timu za vijana.


Hata hivyo, katika moja ya mahojiano ya Mwenyekiti waBodi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ aliyofanya na gazeti hili alisema kocha mkuu na benchi lake ndio watahusika zaidi katika usajili ujao na uongozi uko tayari kufanya matumizi makubwa ingawa wanaamini hawawezi kupata mastaa wakubwa kutokana na muda kuwa mfupi.


“Usajili tutafanya kadri kocha mkuu na benchi lake watakavyotaka. Tupo tayari kuwapa ushirikiano kwa asilimia 100,” alisema Try Again ambaye ni mzoefu kwenye soka la Afrika tangu enzi za Friends of Simba ambalo ni kundi lililokuwa likiendesha mambo mengine klabuni hapo.


Wekundu hao huenda wakafumua asilimia kubwa ya kikosi chao kwenye dirisha hili kwani Benchikha ameonekana kutovutiwa na viwango vya baadhi ya wakongwe ambao wengi ameanza kuwatoa kwenye program zake na viongozi wameanza kumalizana nao kimyakimya.


Simba iliwasili Dar es Salaam jana ikitokea Morocco ilikopoteza mchezo wa makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ikifungwa 1-0 na Wydad Casablanca katika dakika za nyongeza na leo itaanza maandalizi ya mechi ijayo ya ligi dhidi ya Kagera Sugar itakayopigwa Ijumaa hii Desemba 15, kwenye uwanja wenye nyasi bandia wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.