Wakati mastaa wa zamani wa Yanga wakiwataka mabosi wao kuvamia Ghana kwa mshambuliaji Jonathan Sowah fasta na kumsajili, mwenyewe amefungukia kila kitu kuhusu mabingwa hao wa Bara.
Sowah ambaye ni mshambuliaji wa Medeama ya Ghana ameliambia gazeti la Mwanaspoti kwa simu kuwa anajua kwamba Yanga inamhitaji ikivutiwa naye baada ya kucheza mechi baina ya timu hizo iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 nchini humo.
Mshambuliaji huyo alifunga bao la timu yake kwa mkwaju wa penalti akimtungua kipa Djigui Diarra ingawa ndani ya mchezo huo aliwalaza na viatu mabeki wa Yanga kwa ubora wake.
Sowah alisema mara baada ya mchezo huo alifuatwa na baadhi ya watu wa Yanga wakimtaka kuzungumza na rais wa timu hiyo, Hersi Said.
“Najua kwamba Yanga wananihitaji walishanifuata mara tu baada ya ule mchezo pale Kumasi, lakini bado sijaongea nao kwa kina nasubiri simu zao,” alisema Sowah anayevaa jezi namba 3.
“Hakuna mchezaji ambaye anaweza kukataa kujiunga na Yanga. Hii ni klabu kubwa hapa Afrika lakini mimi bado nina mkataba na Medeama nadhani wanatakiwa kuzungumza na uongozi kwanza.
Sowah aliongeza kuwa katika kuifahamu Yanga amekuwa akipokea taarifa nyingi nzuri kutoka kwa beki wao wa zamani Joseph Zutah ambaye yupo ndani ya kikosi cha Medeama.
“Yanga wana timu nzuri kama wangekuwa rahisi wasingetoka siku ile lakini wana ubora mkubwa sehemu zote ni timu iliyokamilika hata mchezo wa marudiano utakuwa mgumu.
“Tangu tulipopangwa kwenye kundi moja nilikuwa napata taarifa mbalimbali zao. Tumekuwa tukiangalia mechi zao lakini hapa kuna mchezaji mwenzetu Zutah (Joseph), aliwahi kupita hapo huwa anatuambia mambo mazuri ya hapo Tanzania hasa kuhusu Yanga na mashabiki wake.”
Mshambuliaji huyo ambaye alikosekana kwenye michezo ya mwanzoni ya hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa amekuwa akiitwa mara kwa mara kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ghana.