UKWELI MCHUNGU: Ishu ya Aucho Bado Tunaadhibu Marefa Badala ya Kutibu Tatizo

UKWELI MCHUNGU: Ishu ya Aucho Bado Tunaadhibu Marefa Badala ya Kutibu Tatizo


Picha za marudio zinamuonyesha kiungo wa Yanga, Khalid Aucho akitaka kuokota mpira ili aurushe. Wakati anainama kuukota, kiungo wa Coastal Union, Ibrahim Ajibu anaudokoa mpira kwa mguu na kuusogeza mbali na mikono ya Aucho.


Kwa hasira, Aucho ananyanyua konga lake la mkono wa kushoto kwenda kichwani mwa Ajibu. Baada ya sekunde chache, Ajibu anajifunika sura kwa mikono miwili na kuanguka chini. Refa hajaona lakini anapogeuka anamjuona Ajibu akigalagala chini huku Aucho akiondoka eneo la tukio.


Refa hajui afanye nini. Baada ya muda, mwamuzi wa akiba anamuita na kuongea naye. Refa anarudi akionekana hana uamuzi lakini baadaye anawaita wachezaji wote wawili na kuwaonyesha kadi ya njano. Kinachofuata ni mijadala redioni, kwenye televisheni na mitandaoni ikimshutumu refa kwa kutoa kadi ya njano kwa Aucho badala ya nyekundu licha ya kutoliona tukio.


Lakini kinachofuata kikubwa zaidi ni cha wale waheshimiwa ambao huwa na maelezo machache kabla ya kutangaza adhabu dhidi ya refa; “kwa sababu ya kushindwa kutafsiri sheria namba xxx” na hapo hufuata adhabu ya ‘kumkomoa’.


Na baada ya hapo hakuna kingine kitakachofuata dhidi ya makosa ya waamuzi hata kama yanajirudia vipi. Wala hataibuka hata mwamuzi wa zamani kuonyesha kushangazwa na kukithiri kwa maamuzi mabovu ya aina fulani. Kitakachofurahisha mashabiki na kuona refa aliyeonekana kufanya maamuzi yaliyoinufaisha Yanga ameadhibiwa, lakini si kwamba kosa linalojirudia limepatiwa ufumbuzi.


Kesho mashabiki wa Yanga watafurahia kuona refa aliyefanya maamuzi yaliyoinufaisha Simba ameadhibiwa na wala si tatizo lililosababisha timu moja inufaike limetatuliwa. Hapo matatizo ya waamuzi yatakuwa yametulia kwenye mzani wa macho ya mashabiki na vivyo hivyo kupunguza lawama kwa mamlaka ya mpira.


Wiki tuliyoimaliza Waingereza walikuwa wakijadili matatizo makubwa ya uamuzi yaliyosababisha timu za Arsenal na Liverpool kuathirika na matumizi mabovu ya Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R).


Liverpool ililalamika na hata kutaka yafanyike mabadiliko makubwa katika uamuzi baada ya bao la Luis Diaz dhidi ya Tottenham kukataliwa kwa madai ya kuotea na vigogo hao wa Ulaya kulala kwa mabao 2-1.


Kocha wa Arsenal, Michael Arteta aliuelezea uamuzi kuwa ni wa aibu baada ya Newcastle kufunga bao licha ya mpira kuonekana umetoka kabla ya pasi ya bao hilo. Arteta naye alitaka kufanyike mageuzi katika uamuzi.


Newcastle pia ilinufaika na makosa ya waamuzi wakati ilipokutana na West Ham. Kocha wa West Ham alilalamika kuwa refa wa mchezo huo, John Brooks alitakiwa amtoe kwa kadi nyekundu mchezaji wa Newcastle, Bruno Guimares kwa kupata kadi ya pili ya njano, lakini hakupewa na mchezo ukaisha kwa sare ya mabao 2-2.


Kwa kujua umuhimu wa uwazi katika uamuzi, Kampuni ya Waamuzi wa Mechi za Michezo ya Kulipwa (PGMOL) ilitoa maelezo yake kuhusu tukio la Liverpool ikikiri makosa kufanyika wakati Jopo Huru la Maamuzi Muhimu ya Mechi za Ligi Kuu ya England halikukubaliana na malalamiko ya Arteta ambaye anaweza kushtakiwa kwa kauli zake licha ya kuungwa mkono na wanafamilia ya soka.


PGMOL, na si kamati ya waamuzi, imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kuzungumzia matukio tata ya mechi, huku mara kadhaa ikikiri kuwepo udhaifu katika uamuzi na kuomba radhi walioathirika.


Huu ni ustaarabu unaotakiwa kwenye mchezo unaofuatiliwa na mamilioni ya watu, huku fedha nyingi zikiwekezwa kwa ajili ya malengo tofauti.


Na PGMOL haijaishia kuzungumzia maamuzi tata tu, bali kwenda mbali zaidi kueleza sababu za kasoro hizo ambazo ni pamoja na uchache wa waamuzi wasaidizi wa video.


Katika mechi za karibuni kumekuwepo na uchelewashaji wa hadi dakika saba wakati V.A.R ikirudia tukio moja na baadaye kumuita mwamuzi wa kati ajiridhishe kabla ya mchezo baina ya Chelsea na Tottenham kuendelea. Ulichezwa kwa dakika 112. Tatizo hilo limeelezwa linatokana na waamuzi wa wasaidizi wa video kuwa na uchovu unaosababisha wafululize kusimamia mechi kama ilivyokuwa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati waamuzi wanne wa video walipolazimika kusimamia mechi Jumamosi na Jumapili.


Ili kuanza kutibu tatizo hilo, PGMOL imetangaza nafasi za kazi kwa ajili ya kazi hiyo ya V.A.R na imehamasisha hata wasio na uzoefu waombe na watapatiwa mafunzo.


Tangazo hilo pia limesambazwa kwa waamuzi waliofuzu uamuzi wakihamasishwa wawe wataalamu wa video licha ua kutokuwa na uzoefu wa eneo hilo la matumizi ya teknolojia ya video.


Sifa za waombaji ni pamoja na kuwa na uwezo wa kuwasiliana kwa usahihi katika mazingira magumu, wawe na uwezo wa kutambua wakati gani V.A.R iingilie mchezo na wenye stadi kubwa za mawasiliano.


Huu ni uthibitisho tosha wa watu wasikivu wanaokerwa na uozo wa uamuzi na wanaofanya kila jitihada kupunguza kasoro licha ya kwamba wameendelea kiteknolojia hadi kukaribia kufikia ukamilifu.


Huku kwetu uamuzi mbovu hauonekani kukera mamlaka na badala yake watu wamekariri sharia na kanuni kwa kudhani kuwa ndizo pekee zinaweza kuondoa tatizo la maamuzi mabovu. Uamuzi mbovu ni tatizo la kibinadamu ambalo likiachwa linaweza kukomaa na kuwa sugu na hivyo kutoa mwanya kwa wajanja kulitumia kwa maslahi yao binafsi.


Lakini likishughulikiwa kwa dhati na pia mamlaka zikaonyeshwa kukerwa, linaweza kupungua kwa kiasi kikubwa na kuondoa karaha wanayoondoka nayo mashabiki wanaolipia viingilio, kusafiri umbali mrefu na hata kulipia ving’amuzi kwa ajili ya kupata burudani na raha.


Kibaya zaidi kinasababisha ligi izungumziwe kwa mabaya kila baada ya mechi na wakati mwingine baadhi ya timu kuonekana zikinufaika na uamuzi mbovu, kitu kinachoondoa ladha ya mchezo wenyewe.


Hatutegemei kuona hatua kali zikichukuliwa dhidi ya waamuzi badala ya mamlaka kuja na mikakati ya kukabiliana na ubovu wa maamuzi katika mechi zote.


Na hili haliwezi kufanywa na vyombo vilevile vilivyozaa tatizo bali vyombo vipya vilivyo nje ya hivi vinavyosimamia mchezo huu kwa sasa. Kama England wana PGMOL, au kampuni huru ya waamuzi, ndivyo sisi tunaonakili tufuate; kwamba chombo huru chenye fikra tofauti ndio kinaweza kufikiria kwa kina nini kifanyike kuokoa fani ya uamuzi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.