Sikia Alichokisema Jean Baleke wa Simba

Sikia Alichokisema Jean Baleke wa Simba


Nyota na kinara wa mabao wa Ligi Kuu kwa sasa, Jean Baleke wa Simba amevunja ukimya na kusema anafurahi kuona anakaribia kufikia idadi ya mabao aliyofunga msimu uliopita, lakini kiu yake ni kufikia au kuzipita rekodi za ufungaji bora wa ligi hiyo zilizowahi kuwekwa na wakali waliowahi kutamba nchini.


Bakele aliyesajili kwenye dirisha dogo la msimu uliopita alimaliza msimu huo akiwa na mabao manane, huku msimu huu kupitia mechi nane tu tayari amefunga saba na anaona ana nafasi kubwa ya kufunga mabao mengi yanayoweza kumfanya afikie rekodi ya kufunga mabao mengi kwa nyota wa kigeni iliyowekwa na Meddie Kagere alipokuwa Simba msimu wa 2018-2019.


Akizungumza na Mwanspoti, Baleke alisema ni jambo zuri kwake kuendelea kufunga na matarajio yake ni kuvuka idadi ya mabao ambayo aliyafunga katika msimu uliopita na jambo hilo linawezekana.


“Nitajitahidi kufunga kila ninapopata nafasi, kwani mechi bado zipo nyingi na tayari nina mabao saba. Hii ni sehemu ya kazi yangu na ukiangalia ligi bado ni mbichi kabisa na nimeonyesha wazi kwamba nafunga na nitaendelea kufanya hivyo.”


Baleke alisema pia anajua kuna rekodi kadhaa zilipo mbele yake ikiwamo ya mabao kwa nyota wa kigeni ya Kegere aliyefunga mabao 23 na ile ya mfungaji bora wa muda wote iliyowekwa na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ akiwa na Yanga mwaka 1998 alipofunga mabao 26 iliyoshindikana kuvunjwa, ila atapambana.


Kauli hiyo nyota huyo wa Simba aliyesajiliwa kutoka TP Mazembe ya DR Congo ni kama mkwara flani kwa Maxi Nzengeli na Stephen Aziz Ki wanaokipiga Yanga anaolingana mabao kwenye orodha ya wafungaji kila mmoja akifunga mabao saba hadi sasa, japo wenzake wamecheza mechi tisa hadi sasa.


Baleke amekuwa na wakati mzuri tangu ajiunge na Simba msimu uliopita kwani aliaminiwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyetimuliwa, kama ilivyo kwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Aziz Ki ambaye msimu uliopita alifunga mabao tisa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.