Kocha Gamondi Ataja Sababu za Yanga Kupoteza Mchezo wa Kimataifa, Aitaja Al Ahly

 

Kocha Gamondi Ataja Sababu za Yanga Kupoteza Mchezo wa Kimataifa, Aitaja Al Ahly

Wakati Yanga ikirejea leo alfajiri ikitokea Algeria, kocha wao Miguel Gamondi amesitisha kutoa mapumziko kwa wachezaji wake huku akifichua siri ya kupoteza mechi yao dhidi ya CR Belouizdad juzi ni wachezaji wake kujisahau.

Yanga ilipoteza mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi mbele ya CR Belouizdad ya Algeria kwa mabao 3-0 na sasa watakutana na bingwa mtetezi Al Ahly ya Misri, mchezo utakaopigwa Desemba 2 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili Gamondi alisema makosa madogo ambayo waliyafanya kwa kushindwa kuzingatia nidhamu ya mchezo ndio yaliyozalisha matokeo hayo.

Gamondi alisema wamepoteza mchezo wa kwanza lakini hawajapoteza malengo yao kwenye mashindano na wanarudi kambini haraka kujiandaa na mechi inayofuata.

“Tulifanya makosa makubwa matatu, nadhani ndio hayo ambayo yamewapa ushindi wenzetu, ni makosa ya kushindwa kucheza kwa nidhamu ya mchezo, hayo ndiyo matokeo ya soka wakati mwingine unaweza kucheza vizuri lakini matokeo akapata mpinzani,” alisema Gamondi.

“Hatuna muda wa kupoteza, tunarudi kujiandaa na mchezo ujao, tutakwenda kukutana na timu nyingine bora, hatuna budi kusahau yote ya mchezo huu kwani ile ni mechi nyingine dhidi ya timu nyingine.

“Tunarudi moja kwa moja kambini kuanza maandalizi, hakutakuwa na muda wa kupumzika, tumezungumza na wachezaji tutarudi eneo la mazoezi kujipanga ili makosa kama haya yasijirudie.”

Aidha kukosekana kwa kipa wao namba moja, Djigui Diarra katika mchezo huo, kocha huyo alisema ni kutokana na maumivu ambayo aliyapata tangu walipocheza dhidi ya Simba.

Hata hivyo, Gamondi alieleza kuna uwezekano kipa huyo akarudi katika mchezo huo ujao lakini madaktari wataendelea kuangalia maendeleo yake.

“Nafikiri hii sio mechi ya kwanza kwa Diara kukosekana, tulimkosa pia tulipocheza dhidi ya Coastal Union, ni baada ya kuumia ile mechi dhidi ya Simba, tuliona tumpe mapumziko ili awe sawa, anaweza kupatikana, itategemea na madaktari ushauri wao katika hizi siku zilizosalia.”

Kwenye mchezo wa huo wa juzi Yanga ilimpa nafasi kipa Metacha Mnata baada ya Diarra kuwa nje huku Aboutwalib Mshery akianzia benchi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad