Mashabiki Wamvaa Refa, kisa Mbwana Samatta
Teknolojia ya usaidizi wa video kwa waamuzi maarufu kama VAR imemtibulia bao nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kwenye mchezo wa Europa Conference League usiku wa Alhamisi kati ya chama lake dhidi ya Eintracht Frankfurt ya Ligi Kuu Ujeruman ‘Bundesliga’.
Samatta aliyeanza kwenye kikosi cha kwanza cha PAOK kama mshambuliaji wa mwisho, alitikisa nyavu za Wajerumani hao katika dakika ya 16, lakini mwamuzi wa mchezo huo, Simone Sozza kutoka Italia alilikataa na kuonekana aliotea kabla ya kufunga.
Mashabiki wa PAOK walionekana kumvaa mwamuzi huyo wa mchezo kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii na wapo ambao waliona bao hilo walinyimwa tu na wala hakuna mchezaji aliyeotea.
“Hakuna lolote hapo ni bao la wazi hilo, wivu tu,” alisema Alexandros, mwingine alidai Samatta hakuwa na bahati ndio maana bao hilo lilikataliwa licha ya kuwa na mchezo mzuri.
Hata hivyo, dakika ya 12 baadaye PAOK ilijipatia bao la kuongoza kupitia kwa Andrija Zivkovic kabla ya Frankfurt kusawazisha kupitia kwa Omar Marmoush ikiwa ni dakika chache kabla ya Samatta kutolewa.
Kocha wa PAOK, Razvan Lucescu alifanya mabadiliko hayo ili kuona kama wanaweza kuvuna pointi tatu kwenye mchezo huo, hesabu hizo zilijipa katika dakika za jioni kabisa 90+2 baada ya Konstantinos Koulierakis kupachika bao la ushindi kwa wababe hao wa soka la Ugiriki.
Kwa matokeo hayo, wamekwea hadi kileleni mwa msimamo wa kundi G la Europa Conference League wakiwa na pointi sita, kituo kinachofuata kwao ni Scotland ambako watacheza dhidi ya Aberdeen, Oktoba 26.