Kuhusu Ishu ya Robertinho Kufukuzwa Au Kuachwa TIMU ya Simba, Saffih Dauda Afunguka
Tangu jana nimekuwa nikifatilia sana mijadala inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii, licha ya Simba kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo wanalalamika wakitaka Kocha (Roberto Oliveira) afukuzwe.
Kwa nini Kocha afukuzwe? Simba imefuzu kwenda hatua ya makundi, hawaangalii katika timu 16 zilizofuzu hatua ya makundi msimu uliopita ni timu nane (8) tu ambazo zimefuzu tena hatua ya makundi, nane (8) nyingine zimekwama.
Simba tangu imeanza kuingia kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika imezidi kupanda kwenye klabu bora. Msimu huu ipo kwenye pot namba mbili [2]. Kwao ni mafanikio makubwa kwa sababu walianzia pot namba nne (4), wakaingia namba tatu (3) na sasa namba mbili.
Simba imeendelea kuwa na mwendelezo, kuna usemi usemao ‘kushika namba moja sio kazi, kazi ni kubaki kuwa namba moja! Huku kwetu ukiendelea kubaki juu watu wanakuzoea na kukuchukulia poapoa.
Yanga ambayo imepambana kutoka chini na kufika kwenye daraja ambalo ipo Simba inaonekana ni bora sana kuliko Simba ambayo ipo hapo kwa misimu kadhaa.
Kuna watu hawaoni kwamba Simba ni timu bora na imeendelea kuwa bora kwenye mashindano inayoshiriki. Imefuzu makundi kwa kuitoa Power Dynamos lakini kwakuwa haijashinda 3-0 watu wanapuuza!
Simba haijashuka ubora ila Yanga imepanda na kufika kwenye daraja la ilipo Simba, lakini watu wanaiangalia Yanga kwa sababu imeifikia Simba lakini Simba imebaki palepale ndio maana wengi wanaona Simba imeshuka.
Simba ipo kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imeshinda mechi zote za Ligi Kuu msimu huu, ubovu wake upo wapi?