Hawa ndio wanaomuangusha Gamondi pale Yanga

Hawa ndio wanaomuangusha Gamondi pale Yanga


Nafurahishwa na wanachopatiwa washambuliaji wa Yanga lakini siridhishwi na wanachokifanya. Kenedy Musonda, Clement Mzize na hata Konkoni walipaswa kutoa zaidi ya walichofanya hadi sasa. Walipaswa kuwa na namba nzuri zaidi.


Yanga wanatengeneza nafasi nyingi na kufunga mabao mengi wanapopata nafasi lakini washambuliaji wao bado wanakosa nafasi nyingi sana. Kuna ukatili wanaokosa Kenedy Musonda na Mzize mbele ya lango.


Zile pasi za mwisho za Aziz Ki na Pacome pamoja na zile krosi za Lomalisa na Yao jeshi, ni pepo ambayo mshambuliaji yoyote anaweza kuiota. Hautapata timu nyingi Afrika zinazotengeneza nafasi kama Yanga.


Ni sababu hii inanifanya nimuelewe kocha wa Yanga anaposema anahitaji kuongezewa wachezaji kuelekea katika hatua ya makundi ya klabu bingwa. Japo kocha hajasema nadhani atakuwa analifikiria zaidi eneo lake la umaliziaji.


Yanga wanahitaji mshambuliaji wa katikati mwenye jicho zuri zaidi la bao. Mviziaji anayeweza kulitawala box la mpinzani na kuamrisha mabeki. Sidhani kama wanahitaji mshambuliaji anayejihusha sana na mchezo. Wanahitaji mviziaji zaidi lakini anayeweza kumalizia vema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.