Fei Toto Afunguka ishu ya Ugali na Sukari "Mpenzi Wangu Ameniacha Kisa Yanga"

Fei Toto Afunguka ishu ya Ugali na Sukari "Mpenzi Wangu Ameniacha Kisa Yanga"
FEI TOTO


Msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kama kuna tukio gumu lililowahi kutikisa nchini ni juu ya sakata la aliyekuwa kiungo wa Yanga Feisal Salum 'Fei Toto' aliyekuwa anashinikiza kuachana na klabu yake hiyo akatue Azam FC.


Takribani miezi nane ya mvutano huo kila upande ukiona uko sahihi huku Fei Toto akikutana na viunzi vigumu tofautitofauti hatimaye kila kitu kilifikia tamati baada ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeziagiza pande zote mbili kukaa na kumalizana.


Fei Toto sasa yuko Azam FC akiendelea na maisha baada ya kuachana na Yanga na baada ya sakata hilo kupita Mwanaspoti limemtafuta na kufanya naye mahojiano maalum kiungo huyo fundi uwanjani akifunguka mambo mbalimbali.


MAISHA MAPYA NDANI YA AZAM


Fei Toto anaanza kwa kuelezea jinsi alivyoanza maisha mapya ndani ya Azam FC akisema kila kitu kinakwenda sawa wakiendelea kuimarika taratibu.


"Maisha mapya ni mazuri tunamshukuru Mungu mpaka sasa hivi tunaendelea vizuri tukiipigania klabu yetu, nadhani taratibu tunaendelea kuimarika kama timu tukiwa na benchi jipya la ufundi na sisi wapya tukitafuta muunganiko bora na wale wenzetu tuliowakuta,"anasema Fei.


AZAM NI TIMU YA AINA GANI


"Azam ni timu nzuri kwangu kwa sababu hata kama nimetoka kwenye klabu nyingine kubwa nadhani nimekuja kwenye klabu kubwa pia kwa hiyo nafurahia maisha mapya nikiwa ndani ya Azam, kila kitu kipo sawa kwangu sioni kitu kilichopungua.


"Akili yangu sasa ni kuipigania Azam najua timu yangu inahitaji nini kutoka kwangu, kitu muhimu ni ushirikiano ambao nimeupata tangu nimefika hapa tuko kama familia moja tunaendelea na majukumu yetu yaliyotufanya kukutana hapa.


AMEPUNGUZA KILO SITA


Baada ya Fei kuwa nje kwa muda bila kucheza mpira akiwa anashinikiza kuhamia Azam baada ya kurudi uwanjani alionekana kuongezeka uzito, hapa anaeleza jinsi alivyopambana kuhakikisha anapungua.


"Ni kweli uzito uliongezeka wakati nafika hapa Azam nilikuwa na kilo kama 75, sikuwa na ratiba nzuri ya mazoezi nilikuwa nacheza au kufanya mazoezi kawaida hasa mwenyewe lakini baada ya kufika Azam na kufanya mazoezi nimeendelea kupungua hivi sasa nina kilo 69 bado naendelea kupambana.


"Kwasasa hapa nilipofika nauona mwili pia mwepesi tofauti na pale mwanzo wakati nafika hapa lakini bado nataka kupungua kidogo zaidi ili nizidishe wepesi.


CHANGAMOTO YA USHINDANI NDANI YA AZAM


"Changamoto ni kubwa hapa Azam kila mchezaji ana ubora mkubwa kwahiyo siwezi kusema jina langu litanipa nafasi kila mchezaji anapambana ili kumshawishi kocha na pia kuisadidia timu najituma ndio maana napata nafasi.


BADO ANAAMINI ATARUDI STARS


Baada ya kutua Azam Fei aliachwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ambacho kilikwenda kukata tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa Afrika kule nchini Algeria hapa anaeleza jinsi alivyopokea maamuzi ya kocha Adel Amrouche.


"Kushtuka ni kawaida kwa kuwa mimi ni Mtanzania lakini niliichukulia kawaida na kuifanya kuwa changamoto kwangu, unajua kocha ndiye anayejua mipango yake jukumu langu ni kuheshimu maamuzi ya kocha, wala siwezi kumpinga ninachofanya ni kuendelea kupambana, hata kama sikuwepo lakini niliendelea kuliombea taifa langu lifuzu naamini Mungu akitupa uhai nitarudi tu kwenye timu.


ZOMEA ZOMEA YA MASHABIKI WA YANGA


Baada ya kutua Azam Fei amekuwa akikutana na zomeazomea kutoka kwa mashabiki wa timu yake ya zamani ya Yanga kama ambavyo ilimtokea pale Mkoani Tanga wakati Azam ilipokutana na timu yake hiyo.


"Mashabiki kuzomea au kunizomea mimi ni kitu cha kawaida hilo nililijua litanitokea nilishajiandaa kiakili unajua matukio ya namna hii hata Ulaya yapo kwa mchezaji anapohama timu moja kwenda nyingine siku wakikutana atazomewa tu, kwangu mimi niliwapotezea na kujikita kufanya kazi yangu uwanjani wala sina shida nao.


PRESHA YA KUKUTANA NA YANGA


"Kukutana kwa mara ya kwanza na timu uliyotoka kama mchezaji lazima utakuwa na presha siwezi kusema sikukutana nayo, bahati mbaya matokeo hayakuwa kwa upande wetu, iliniumiza kwa kuwa mimi sasa ni Azam na ndiyo timu iliyopoteza mchezo, niliyapokea matokeo na kuangalia mbele ile mechi ilishapita.


ALIWAZA NINI KABLA YA MECHI?


"Kabla ya mechi nilikuwa nawaza mambo mengi lakini kiujumla niliona kwamba itakuwa mechi ngumu na yenye presha, nilijipanga kufanya kile ninachoweza kuisaidia timu yangu bahati mbaya Mungu hakutuwezesha kupata matokeo tuliyoyataka tunamshukuru kwa hilo ipo siku wakati wetu utakuja.


ILE PICHA KASHIKA KICHWA


Baada ya ushindi wa Yanga hasa wapinzani wao kupata bao la pili kuna picha moja ilizunguka ikimuonyesha Fei toto ameshika kichwa huku Yanga wakishangilia hapa anaeleza ilivyo muumiza.


"Ile picha niliiona baadaye baada ya mchezo kiukweli iliniumiza sana kama mchezaji unajua ilikuwa inatumika kama kebehi kwangu na maneno mengi lakini ndio soka hakuna namna niliyapokea yote."





FEI TOTO ATARUDI TU


"Kwasasa ni kama mtu ukihamia nyumba mpya kuna namna unahitaji kuutafuta utulivu ukiwa makazi mapya ndani ya timu yangu pia naamini mambo yatakuja kutulia na muda sio mrefu na Feisal ni yuleyule atarudi kwa haraka sana watu wangu watulie, unajua kukaa nje takribani miezi nane bila kucheza soka la ushindani sio kitu kidogo ni hatua mbaya kwa mchezaji ila taratibu nitarudi.


ALETEWA KOCHA MAALUM


"Nawashukuru sana Azam FC kwa maana ya uongozi na kocha walijua ni huduma gani nahitaji kuipata baada ya kurudi uwanjani, tukiwa kwenye maandalizi ya msimu mpya kule Tunisia nililetewa kocha maalum wangu binafsi wa kunipa mazoezi sahihi yatakayonirudisha uwanjani, alipomaliza kazi yake akaondoka na sasa naendelea na makocha wa timu yangu, nashukuru Mungu juhudi hizo ndizo zilizonifanya nicheze sasa.


SAKATA LA KUHAMA YANGA LIMEMPA FUNZO


"Kiukweli ule ulikuwa wakati wangu mgumu ambao sikuwahi kudhani ningeupitia kwenye kucheza kwangu mpira lakini kuna funzo kubwa nimelipata kwamba unapokuwa mchezaji kuna maisha unatakiwa uwe nayo makini hasa mambo ya mikataba ni vyema kila mchezaji akawa na msimamizi sahihi wa mambo ya mikataba.


AKIMBIWA NA MPENZI WAKE


"Lile sakata liliniathiri kwenye mambo mengi sana sio kwa upande wa kucheza pekee, wakati niko kwenye wakati mgumu kama ule kila wakati unafikiria hii kesi itaishaje, nikakutana na pigo lingine la kukimbiwa na mpenzi wangu ambaye niliamini ningekuja kumuoa.


"Aliona kama maisha yangu ya soka tena basi ndio yameishia pale alishindwa kuvumilia na kuamua kutafuta mtu mwingine kitu kilichoniumiza zaidi ni hatua mbaya zaidi kwangu ikawa kwenda kuolewa tena nikiwa katikati ya lile sakata, sikuwa nimemuoa ila tulikuwa na mipango mingi ya maisha kati yetu, hakutaka kuvumilia kabisa nililazimika kuyapokea maamuzi yake hakukuwa na namna na sasa nimerudi uwanjani maisha mengine yataendelea tu."


HAKUMTAFUTA BAADA YA SAKATA KUMALIZIKA


"Hapana hakunitafuta na wala mimi sikumtafuta nilikubaliana na maisha au maamuzi aliyoyachukua na bahati mbaya sana mimi huwa sina hulka ya kuangalia nyuma eneo ambalo nimeondoka nilikubaliana naye maisha lazima yaendelee kwake na kwangu nikipata mwingine nitashukuru Mungu.


ISHU YA UGALI NA SUKARI


Fei aligoma kueleza kwa undani ile kauli ya kwamba alipokuwa Yanga alikuwa anakula ugali na sukari madai ambayo yaliibuliwa na mama yake mzazi akibaki anacheka huku akisema kwa kifupi


"Unajua ugumu wa jambo flani hakuna ambaye atalijua kwa undani zaidi ya yule aliyelipitia mimi siwezi kumzuia mtu kusema kitu lakini namshukuru Mungu hili limepita salama niliamua kupuuza baadhi ya mambo ili maisha yaendelee.


ULIKUWA WAKATI SAHIHI KUONDOKA YANGA?


"Huu ni mchezo wa mpira kila kitu kinatokea kwa wakati husika, nafikiri ile nafasi ya kuondoka ilikuja wakati ule na sikuwa na namna zaidi ya kufanya maamuzi yatakayolenga kuangalia kesho yangu, watu wanatakiwa kufahamu maisha ya soka ni kwa kipindi kifupi sana ukisema uangalie ushabiki basi baada ya muda wako wa kucheza utakuja kuumbuka binafsi niliona baada ya maisha yote niliyoishi Yanga nilitakiwa kuondoka kwa kuiangalia kesho yangu zaidi.


ELIMU YAKE KWA WANAOCHIPUKIA


"Wapo wengi ambao walicheza mpira kabla yetu tunaweza kupata nafasi ya kujifunza maisha yao ya sasa, tunawaona ambao wanaishi vizuri wachache na wengine maisha yao tunayaona pia wito wangu kwa wachezaji wenzangu wanaocheza sasa na wengine watakaokuja watambue mpira ni kitu cha muda mfupi sana, mashabiki wanabaki lakini wachezaji tunapita kwa hiyo kila mmoja afanye maamuzi kwa maisha yake, kitu bora zaidi nisisitize ni juu ya kuwa na wasimamizi sahihi hili wenzangu walichukulie kwa uzito, tuache kuchukulia mambo kirahisi yana ugumu wake baadaye.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad