Kocha Kaze Mbona Ghafla sana

 

Kocha Kaze Mbona Ghafla sana

Juzi Yanga imetambulisha rasmi kocha msaidizi mpya atakayefanya kazi na kocha mkuu, Miguel Gamondi ambaye ni Moussa N'Daw kutoka Senegal mwenye umri wa miaka 54. Ni mshambuliaji wa zamani wa timu za Wydad Casablanca, Al Hilal, Farense na Al Riyadh na baada ya hapo akagaukia ukocha ambapo timu ya mwisho kuifundisha kabla ya kujiunga na Yanga ni ASC Jeanne d'Arc ya kwao Senegal.


Hapana shaka yoyote kuwa kuingia kwa N'Daw kunamaanisha rasmi kwamba aliyekuwa akihudumu katika nafasi hiyo msimu uliomalizika Cedrick Kaze, hatoendelea tena kuinoa timu hiyo.


Hili wengi tulilitegemea kwani mara nyingi makocha wakuu wanapoingia kwenye timu, huwa ni nadra sana kukubali kufanya kazi na wasaidizi ambao wamewakuta kwenye timu hasa wanapokuwa na wasifu mzuri kama wa Cedrick Kaze.


Sijasema kuwa haiwezekani bali huwa ni mara chache sana, makocha wapya wanapokuja kwenye timu kuridhia kufanya kazi na wasaidizi ambao wamewakuta na hata inapotokea wanakubali, mara kwa mara huwa kunatokea migogoro na utofauti baina yao.


Kwa maana hiyo suala la Kaze kuondoka Yanga baada ya ujio wa Gamondi lilitegemewa na wengi lakini anaondokaje ndio kitu kilichosubiriwa kwa hamu.


Kutokana na mchango na uwajibikaji ambao Kaze alikuwa nao kwa Yanga, tulitegemea kuona klabu hiyo ikimuaga kwa kumpa shukrani kama ilivyofanya kwa Nabi na aliyekuwa kocha wa makipa Milton Nienov ambao kupitia kurasa rasmi za timu, walipewa asante au 'Thank You' kama ilivyozoeleka hivi karibuni.


Lakini imekuwa tofauti kwa Kaze ambaye tumeshtukia tu akiletwa kocha mpya msaidizi pasipo kuambiwa lolote kwamba msaidizi huyo wa Nabi msimu uliopita anaondoka ndani ya Yanga au ataendelea kuwepo au nini kinaendelea kumhusu.


Sijui kwa nini imekuwa ghafla kwa Cedrick Kaze, au watatusapraizi kwa kumpa agano la eshima siku ya kilele cha Wiki ya Mwananchi? Ni suala la kusubiri na kuona.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.