Baada ya Kocha Nareddine Nabi kuondoka ndani ya Young Africans, kiungo wa kati wa timu hiyo, Mkongomani Yannick Bangala amesema kuwa anatamani kumuona kocha mkubwa mwenye uwezo kama alionao Florent Ibenge akiinoa Young Africans kwa msimu ujao.
Bangala amewahi kufanya kazi kwa pamoja na kocha Ibenge ndani ya AS Vita na DR Congo ambapo kwa sasa wawili hao kila mmoja akiwa na timu yake, Bangala akiwa Young Africans na Ibenge akiwa Kocha Mkuu wa Al Hilal ya Sudan.
Bangala amesema kuwa: “Kwanza nimshukuru kocha Nabi kwa kila kitu ambacho amekionyesha ndani ya Young Africans, alikuwa ni mhimili mzuri sana kwetu wote wachezaji, alikuwa ni kiongozi haswa aliyefahamu kuishi na kila mchezaji na akacheza.
“Kwangu mimi kuhusu kocha mpya nafahamu kuwa viongozi wanafahamu nini cha kufanya kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanampata kocha mkubwa na mwenye uwezo wa kuipa timu mafanikio,
“Akipatikana kocha mkubwa kama Ibenge naamini timu itazidi kupiga hatua kwa kuwa ni kocha ambaye anafahamu vizuri soka la Afrika, kwangu Ibenge ni moja ya makocha ambao ni wazuri kwa kuwa amewahi kunifundisha, nitafurahia kumuona Young Africans,” amesema kiungo huyo