Young Africans Akili Kubwa Kombe la Shirikisho, Alama Tatu Zabaki Kubeba Ndoo Ligi Kuu

Yanga

Licha ya kubakisha alama tatu kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Benchi la Ufundi la Young Africans, limesema akili zao zinauwaza mchezo wa Jumatano (Mei 10) dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini.


Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa kwanza wa hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ‘CAFCC’, utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1.00 usiku.


Kwa upande wa Ligi Kuu Bara, Young Africans imebakisha michezo mitatu dhidi ya Dodoma Jiji FC, Mbeya City na Tanzania Prisons, ambapo itahitaji pointi tatu tu kutangaza kutetea ubingwa wake kutokana na pointi zake kutoweza kufikiwa na timu nyingine yoyote.


Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 71, imeshinda michezo 23, imefungwa na kutoka sare michezo miwili miwili wakati ikifunga mabao 52 na kuruhusu kufungwa mabao 13.


Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, amesema kwa asilimia 90 tayari wameunusa ubingwa hivyo akili zao zinahamia katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAFCC’ ambapo wanaamini watakuwa na michezo migumu.


Amesema wapinzani wao ni wazuri na ndio maana wamefika hatua hiyo, wao wanahitaji kufika fainali ya michuano hiyo hivyo utakuwa mchezo mgumu kutokana na kila timu kuitaka fainali.


“Kwa hapa tulipofika hakuna timu nyepesi, tunakwenda katika mapambano, timu kutoka Afrika Kusini ni ngumu lakini tutapambana kwa sababu ya mashabiki wetu wamekuwa wakitusapoti ambao sana kwa kutaka kuona mafanikio ya klabu,” amesema.


Kikosi cha Young Africans kilirejea jijini Dar es salaam jana Ijumaa (Mei 05) jioni kikitokea Singida na leo Jumamosi (Mei 06) kinatarajiwa kuingia kambini kujiandaa na mchezo huo wa Nusu Fainali.


Young Africans imetinga hatua ya Nusu Fainali ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-0 baada ya kuichapa timu ya Rivers United ya Nigeria katika michezo ya Robo Fainali.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.