​Mrisho Ngassa Afunguka Mengi Kuhusu Maisha Yake ya Sasa "Pale Simba Wamepigwa Hakuna Wachezaji"

Mrisho Ngassa


WACHEZAJI wengi siku hizi ambao wamestaafu soka ama wanaelekea kustaafu huonekana wakisomea ukocha lakini hii imekuwa tofauti kidogo kwa winga wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Mrisho Khalfan Ngassa.

Ngassa hajatangaza kutundika daluga ila amepumzika kwa muda kucheza soka la ushindani na sasa ana kituo chake cha kulea na kukuza vipaji vya vijana kinachoitwa Enjoy Soccer Academy ambacho ameajiri kocha huku yeye akiwa mkurugenzi tu.

Kituo hicho kina jumla ya wachezaji 80, kipo Boko Basihaya jijini Dar es Salaam ambapo vijana 30 ni wale wa umri chini ya miaka 17 (U-17) na U-20 wakati vijana 50 wana umri kati ya miaka 10 na 15.

Wengi watakuwa walimuona Ngasa alipokuwa akicheza ingawa baadhi yao huenda wamekuwa wakisoma ama kusikia historia yake tu kwenye soka nchini namna alivyokuwa winga hatari hasa alikuwa Yanga na bado anatajwa kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi timu ya taifa hadi sasa.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Ngassa anaelezea juu ya kituo chake hicho pamoja na mambo kadhaa kwenye soka la Tanzania.


ENJOY SOCCER ACADEMY

Ngassa ambaye soka la ushindani katika timu saba anaeleza zaidi kuhusu kituo chake hicho; "Niliamua kuanzisha kituo hiki ili kurudisha fadhila kwa jamii, njia pekee niliyoona inafaa ni kuwasaidia vijana kutimia ndoto zao kupitia soka.

"Hivyo kwenye kituo changu nina vijana wenye mchanganyiko wa umri ambao baadhi yao wapo timu zinazoshiriki ligi ngazi za chini kama First League.

"Nimewatoa sehemu tofauti na kuna wachezaji kama wanne wanacheza Stand United na wawili wapo Copco United, hapa hakuna wanacholipia, kila kitu nakifanya mimi ingawa uendeshaji ni mgumu kwani sijapata wafadhili bado, huwa natoa pesa kutoka mfukoni mwangu."

Ngassa anaendelea kusema kuwa; "Nina wachezaji watano pekee ambao wanakaa sehemu moja kama kambi kwani hawa wanatoka mbali lakini wengine wote wanatoka makwao, wakifanya mazoezi wanarudi.

"Tanzania ina vipaji vingi, naamini hata kutoka kwenye kituo hiki wataibuka mastaa wa baadaye watakalolisaidia Taifa kisoka, vipaji vipo ila havijaendelezwa, ni muda wangu sasa kuona namna gani nawasaidia."

Kutokana na kituo hicho, Ngassa anaweka wazi kuwa ndicho kilichosababisha apumzike kucheza soka kwa muda.

"Kuna mambo nilikuwa nayaweka sawa kwenye kituo ili nikirudi kucheza basi huku niwe nimetengeza misingi mizuri, nimemaliza kwa asilimia kubwa sasa najipanga kurejea katika ligi msimu ujao.

"Siwezi kusema ni timu nitaichezea ila ifahamike tu kwamba bado sijastaafu soka na msimu ujao mashabiki wataniona nikiwa katika moja ya timu za Ligi Kuu najiamini kuwa bado nina uwezo mkubwa wa kucheza, kikubwa najitunza," anasema Ngassa aliyewahi kuzichezea timu za Kagera Sugar, Yanga (mara tatu tofauti), Azam, Simba, Free State Stars, Fanja, Mbeya City na Ndanda


LIGI KUU ILIVYO/WAGENI

Winga huyo hatari anasema kwamba Ligi Kuu hivi sasa pamoja na ligi zingine kama Championship zimepiga hatua kubwa kutokana na uwekezaji uliopo.

"Mpira umepiga hatua kubwa sana, hivi sasa soka letu limekuwa ajira, wachezaji wanalipwa vizuri na uwekezaji umeongezeka ndiyo maana kuna ushindani mkubwa si ligi kuu wala Championship

"Ndio maana pia tunaona hata wachezaji wengi wa kigeni wanakuja kucheza hapa ingawa baadhi yao viwango vyao ni vya kawaida sana huwezi kutofautisha na wazawa

mfano kama yule Augustino Okrah na Mohammed Quattara pale Simba ni kama walipigwa maana hawajaisaidia timu kama ilivyotarajiwa.

"Wapo wengi tu wachezaji wa kigeni kwenye hizi timu hasa Simba na Yanga wanakuja ila uwezo ni mdogo na wao wanaridhika kwasababu hizo timu ni kubwa Afrika, hivyo wanajua wanaposema wanacheza Simba ama Yanga kwao ni faida kubwa.

"Lakini kuna wale wazawa ambao wanajisahau pale wanapopata mafanikio kidogo inakuwa ndio mwisho wao, hawaupi thamani na ubora wa mpira wao, mchezaji akipiga hat-trick moja hawezi tena kuendeleza uwezo wake kwani analewa sifa jambo ambalo ni hatari kwao.

"Mchezaji unatakiwa kulinda kiwango chako kwa kujiweka tayari hasa kwa wale ambao wapo tu ndani ya timu na kukaa jukwaani, maana ni lazima itafikia muda wataachwa tu, pia ikumbukwe kwamba wengi wanalinda wanachokipata kwenye timu bila kujali viwango vyao hawa nao wanapaswa kuamka."


PESA YA AZAM

Ngasa ni mchezaji wa kwanza kwa miaka yao kuuzwa ndani ya Yanga kwenda Azam FC msimu wa 2010/13 akisaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh 40 milioni.

"Sikuwa mjinga kuondoka Yanga kwenda Azam FC wakati ule, niliangalia pesa waliyoniwekea mezani na nilifuata utaratibu wote. Nilipewa Sh 40 Milioni ambayo nilinunua nyumba kule Yombo kwangu ndicho kitu nilichokiona kinanifaa kwa wakati huo.

"Unapoondoka kwenye timu moja kwenda nyingine unatakiwa kuangalia maslahi yakoje, pamoja na faida nyingine unazokwenda kuzipata huko, lakini hata nilipoenda Simba kwa mkopo nikitokea Azam kuna pesa nililipwa kwa mujibu wa mkataba wangu ulivyokuwa unaeleza ingawa siwezi kusema Simba walinilipa kiasi gani.

"Sikuchagua mimi kwenda Simba ila waajiri wangu ndiyo waliona hivyo baada ya kutokea mambo ambayo wao waliamini kuwa yapo kinyume na wao, sikupinga kwenda Simba kwani mimi ni mchezaji popote nacheza na nilifurahia maisha ndani ya Simba kama kawaida tu,"

Ngassa, aliingia kwenye mgogoro na mabosi wake baada ya kuvaa jezi ya Yanga katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki dhidi ya Azam na AS Vita ya DR Congo alionekana amevaa jezi hiyo aliyopewa na shabiki baada ya mpira kumalizika.

Kwenye mechi hiyo Ngassa alifunga bao lililoipeleka Azam fainali kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Vita SC na kwenda upande wa mashabiki wa Yanga kushangilia na fainali za michuano hiyo ilizikutanisha Yanga na Azam.

“Ile mechi niliingia nikitokea benchi na nilifunga, sasa baada ya bao lile na tukio lililokuwa linazungumzwa wakati natoka nilivalishwa jezi na shabiki, niliona nimalizie, niliwaomba radhi viongozi wa Azam lakini kutokana na maneno ya pembeni hawakuniamini,” anasema.

“Mechi ya fainali kocha Sterwat Hall aliambiwa asinipange kikosini ila nilikuwa benchi, aliniingiza baada ya kuona mambo si mambo, lakini mwisho wa siku tulipoteza ule mchezo niliingia kama dakika 10 za mwisho”.

"Baadaye Hall naye aliondolewa kwani alionekana kwenda kinyume nao na hata mimi nilienda Simba baada ya kujadiliana na Yusuph namna ninavyojisikia kutokana na zile tuhuma kwani alikuwa mtu wangu wa karibu hadi hivi sasa.


ALIYOKUMBANA NAYO SAUZI

Wakati Ngassa anakwenda Free State timu hiyo ilikuwa chini ya Kinnah Phiri raia wa Malawi anayedaiwa kupendekeza usajili wake na aliishi naye kama mwanaye kutokana na kumkubali.

Baadaye kocha huyo aliondoka na kurudi kwao Malawi na hapo ndipo majanga kwa Ngassa yalipoanza kwani kocha aliyeajiriwa alikwenda na wachezaji wake na hivyo Ngassa kutokuwa chaguo lake ingawa pia alikuwa ameumia nyama za paja.

“Nilipoumia akaja kocha mpya, yule kocha alikuja na wachezaji wake wengine wapya, kwa hiyo akawaambia viongozi tu kwamba yeye ana wachezaji wengine wazuri wanaoweza kucheza nafasi yangu.

“Basi kutokana na kuwa na majeraha wale Wasauzi waliamua kuachana na mimi, nikarudi nyumbani nikajitibia na kuwa sawa ndipo nikajiunga na Mbeya City ambayo wakati huo Phiri ndiye aliyekuwa kocha.”

"Kiukweli Tanzania tuna upendo mkubwa sana, yaani tunapenda watu, wenzetu huo hasa Afrika Kusini wanaiona Tanzania kisoka tupo chini sana hivyo wanaonyesha dharau na ubinafsi, kuna ubinafsi mkubwa unaokatisha tamaa." anasema

Ngassa aliwahi kupata dili la kusajiliwa El Mereikh ya Sudan ambayo iliahidi kumpa fungu la maana lakini hakusaini dili hilo kwa madai kwamba Yanga tayari walikuwa wamempa donge nono baada ya kumaliza mkataba wake wa mkopo na Simba.

“Kikubwa ni kuwa mwaminifu, nisingesaini wakati tayari nimesaini na timu nyingine, nisingeeleweka."

Hata hivyo, Phiri aliyewahi kumfundisha Ngassa timu mbili tofauti aliliambia Mwanaspoti kuwa; "Ngassa ni mchezaji mzuri, nimeishi naye kama mwanangu ila maisha ya Afrika Kusini yalimshinda kutokana na mambo mengi yaliyotokea ndani ya timu baada ya mimi kuondoka.

"Achana na mambo ya ujana, ila Ngassa alikuwa winga bora, kazi yake alijua kuifanya vyema ndiyo maana alipoondoka kule nilimchukuwa Mbeya City lakini wanasema wakati ni ukuta, kila kitu kina mwisho ni lazima wazaliwe akina Ngassa wengine," anasema Phiri

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad