Singida Big Stars juzi jioni ilifumuliwa mabao 2-0 na KMC kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini tayari mkononi ina tiketi ya michuano ya kimataifa kwa msimu ujao na katika kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa huko, imeanza kusajili kimya kimya na sasa imehamia kwa Bernard Morrison 'BM33'.
Mbali na winga huyo Mghana aliyefunga bao la pili la Yanga, walipoizamisha Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa mabao 2-0 katika pambano la kwanza la nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, pia Mzambia anayekipiga Simba kwa sasa Moses Phiri naye anatajwa kunyemelewa Singida.
Inaelezwa kuwa, BM33 yupo hatua ya mwisho ya kukamilisha dili la kutua Singida Big Stars kwa dili lake limeanza mapema kulinganisha na la Phiri ambaye anatajwa tu, bila kuelezwa kama ameanza kuzungumza na mabosi wa klabu hiyo inayonolewa na kocha Mholanzi, Hans Pluijm.
Singida imejihakikishia kumaliza ndani ya Nne Bora ya Ligi Kuu ikiichezea kwa msimu wa kwanza baada ya kupanda kutoka Ligi ya Championship, huku ikiwa nusu fainali ya Kombe la ASFC na hivyo kushikilia tiketi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika sambamba na Azam, Simba na Yanga.
Katika kuhakikisha inajipanga mapema kwa michuano hiyo ya CAF inaelezwa viongozi wa Singida tayari wameanza usajili wakianza na Kakolanya anayemaliza mkataba wake na Simba na sasa imemgeukia Morrison ambaye naye mkataba wake na Yanga upo mwishoni kumalizika.
Inaelezwa benchi la ufundi limeanza mapema mchakato wa kukiboresha kikosi hicho wakitaka kuongeza kundini wachezaji wenye uzoefu wa michuano hiyo na miongoni mwao ni BM33 aliyewahi kuzichezea AS Vita na DC Motema Pembe za DR Congo na Orlando Pirates ya Afrika Kusini kabla ya kuja Tanzania kujiunga na Yanga na baadaye kuhamia Simba na kisha kurudi Jangwani.
Taarifa kutoka ndani ya Singida zinasema kuwa, dili la Morrison limekuwa rahisi kwa vile winga huyo hayupo kwenye mipango ya Kocha Nasreddine Nabi pale Jangwani kutokana matukio mengi huku mkataba ukikaribia kumalizika bila mabosi wa Yanga kutaka kumuongezea mpya kwa sasa.
Licha ya kwamba Singida BS inakabiliwa na upinzani kutoka kwa Azam FC, wapo mbele kwenye vita ya kupata saini yake na tayari walishafanya mazungumzo na mchezaji huyo ambaye anafurahia maisha yake ya soka nchini.
Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa Singida aliyekata kutajwa jina gazetini alisema kilichosalia kwa mchezaji huyo ni kuwekewa fedha tu kwani kila kitu kimekamilika na amepewa mkataba wa awali wa msimu mmoja tu.
"Ishu ya Morrison ilipofikia sidhani kama kunaweza kutokea mabadiliko yoyote ni kuhakikishie utamuona msimu ujao akiwa na timu yetu, ni mchezaji mkubwa ambaye tunaona anaweza kutusaidia," kilisema chanzo hicho na kuongeza;
"Tumekuwa na mazungumzo naye karibu mara tatu hadi nne na jambo zuri kwetu tulipoongea na kocha wetu juu ya usajili wake alipitisha na kusema ni mchezaji ambaye anaweza kuongeza nguvu kwenye timu."
Mbali na Morrison, mchezaji mwingine ambaye anatajwa kuwa kwenye rada za Singida BS ni pamoja na kinara wa mabao wa Simba kwenye ligi, Moses Phiri ambaye kwa sasa hana furaha kwenye kikosi cha Roberto Oliveira 'Robertinho'.
Inaelezwa Phiri mwenye mabao 10 kwenye ligi tayari amewasilisha maombi ya kuondoka mwishoni mwa msimu kutokana na kukosa kwake nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi hicho chini ya Robertinho ambaye ameonekana kuwa na imani zaidi na Jean Baleke ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali.