Manula; Kutoka mshahara wa Tsh 150,000 mpaka mil 1.5

Manula; Kutoka mshahara wa Tsh 150,000 mpaka mil 1.5


Kipa namba moja wa Klabu ya Simba na Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Aishi Salum Manula amesema kuwa mshahara wake wa kwanza baada ya kuajiriwa na Azam FC ilikuwa Tsh 150,000.


Manula amesema hayo wakati akifanyiwa mahojiano maalum na Millard Ayo akizungumzia historia ya maisha yake ya soka.


“Baada ya kujiunga na Azam Academy, Septemba 2011 nikitokea mashindano ya Copa Coca Cola na timu yangu ya Kilombelo nikiwa kidato cha pili, nilihama shule nikarudi Dar na kujiunga na Mbande Sekondari ya Chamazi.


"Novemba mwaka huo huo kukawa na mashindano ya vijana yaliitwa Uhai Cup yaliyojumuisha timu zote za Under 20 za Ligi Kuu, nilifanya vizuri sana nikawa kipa bora wa mashindano na tukabeba ubingwa.


“Novemba hivyo hivyo nikapandishwa kutoka Under 20 kwenda timu kubwa (senior team) ya Azam chini ya Kocha Stewart Hall. Desemba Azam tukaenda kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar.


“Januari ya 2012, ndipo nikaanza kulipwa mshahara ambao ulikuwa ni Tsh 150,000 kwa mwezi nikiwa timu kubwa, ilikuwa kitu kikubwa sana kwangu. Pia nikaitwa Timu ya Taifa ya Under 20 kama kipa namba moja lakini Azam FC nikiwa kipa namba 2 na kipa namba moja alikuwa Mwadini Ally mimi nikiwa benchi.


“Mwaka huo huo 2012 nikapandishwa mshahara mpaka tsh 500,000 kutokana na uwezo wangu, nikampeleka mdogo wangu shule ya biafsi ya boarding na kuanza kumlipia ada. Azam ilikuwa kama una-perform vizuri unaongezwa mshahara hata kama mshahara wako haujamalizika.


“Mwaka 2013 ndipo nikaanza kucheza rasmi timu kubwa na ndio msimu ambao Azam FC inahukua ubingwa kwa mara ya kwanza na mimi nikiwa langoni. Mwaka 2014 nilipewa mkataba mpya wa miaka mitatu na signing fee ya Tsh milioni 30 na mshahara wa Tsh milioni 1.


“Nilienda kucuhukua pesa hiyo ofisini pale Mzizima nikahisi kama watu wananiona, kila nikipanda dal;adala nashuka nahisi kuibiwa, nikapanda pikipiki mpaka benki nikaziweka. Baadaye nilianza taratibu za kununua kiwanja na kuanza kujenga. Baadaye nikaongezewa mshahara mpaka Tsh milioni 1.5 ambao mpaka nikamaliza mkataba.


“Baada ya kumaliza mkataba Simba walinifuata tukafanya nao mazungumzo, tukafikia muafaka nikajiunga na Msimbazi mwaka 2017 mpaka leo,” amesema Manula.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.