Kocha Simba SC aomba radhi, kukutana na uongozi

Published from Blogger Prime Android App


Hatimaye Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo ‘Robertinho’, amewaomba radhi Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo, baada ya kikosi chake kushindwa kutinga Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

Simba SC ilipoteza 2-1 mbele ya Azam FC juzi Jumapili (Mei 07) katika mchezo wa Nusu Fainali uliochezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Kocha Robertinho amesema anatambua matokeo hayo yamewaumiza Mashabiki na Wanachama wa Simba SC, hivyo hana budi kutoa neno la kuomba radhi kwa sababu kilichotokea hakikuwa kusudio la wengi ambao walitamani kuiona timu yao ikienda Fainali ya ASFC.

Amesema licha ya kupoteza mchezo, bado kikosi chake kilionesha kupambana ili kusaka ushindi dhidi ya wapinzani wao Azam FC, lakini bahati haikuwa kwao, na sasa wamebaki mikono mitupu kwa msimu huu 2022/23.


“Haya mambo yanatokea kwenye mpira, matokeo yameumiza Wanasimba wote, pamoja na kucheza vizuri hatukuwa na bahati, tulitengeneza nafasi nyingi lakini hatukuzitumia vizuri…, kwenye mchezo kama huu unaohitaji matokeo unapaswa kutumia vema kila nafasi unayoipata, niwaombe radhi mashabiki wa timu yetu kwa matokeo haya ambayo hatukuyategemea,” amesema Robertinho

Amesema kama kiongozi wa Benchi la ufundi atakutana na uongozi wa klabu hiyo kuangalia nini cha kufanya kuhakikisha msimu ujao wanarudi kwa kasi kubwa.

Wakati huo huo Meneja Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally umekiri kuwa hakuna hatua waliyopiga msimu huu kutokana na kuondolewa kwenye mashindano yote huku wakiwa hawana uhakika wa ubingwa wa Ligi Kuu.

Ahmed, amesema kuwa hakuna walichoongeza kulinganisha na msimu uliopita ambapo kwenye michuano yote waliishia hatua waliyoishia msimu huu.

“Msimu uliopita kwenye mashindano ya CAF tuliishia hatua ya robo fainali kama ilivyo msimu huu, lilikuwa kufika angalau nusu fainali, kwenye michuano ya FA tuliishia nusu fainali sawa na msimu huu, tulipoteza ubingwa wa Ligi Kuu na msimu huu dalili ni hizo hizo, ukiangalia hapo na kulinganisha utaona hakuna hatua tuliyopiga,” alisema Ahmed.

Kutokana na hayo amesema uongozi wa klabu hiyo utakaa na kuangalia aina ya wachezaji walionao na kuona wapi wanatakiwa kuboresha ili msimu ujao wavuke walipoishia misimu miwili mfululizo.

“Lazima tuwe na wachezaji ambao wanauwezo wa kututoa hapa tulipo kufika mbele zaidi, uongozi na benchi la ufundi utakaa na kuliangalia hili kwa kina, tutarudi kwa kishindo kikubwa msimu ujao,” amesema Ahmed.


Msimu huu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba SC waliondolewa hatua ya Robo Fainali na Wydad Casablanca ya Morocco huku kwenye ligi ikiwa imezidiwa kwa alama saba na wapinzani wao, Young Africans walioukaribia ubingwa huku ikiwa imebaki michezo mitatu kabla ya ligi kumalizika.

Young Africans wanahitaji ushindi kwenye mchezo mmoja tu kati ya hiyo kutwaa ubingwa msimu huu 2022/23.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.