ALIYEWAHI kuwa Kocha Msaidizi wa Yanga na kocha wa viungo wa Mamelod Sundowns, raia wa Afrika Kusini, Riedoh Berdien amewatazama wapinzani wa Yanga kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Marumo Gallants na kuwaonya Yanga kuwa wanapaswa kucheza kwa tahadhari kubwa kama wanataka kutinga fainali.
Yanga keshokutwa Jumatano wanatarajiwa kuwa wenyeji wa Marumo Gallants katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, mchezo ambao unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Baada ya mchezo huo Yanga watasafiri mpaka Afrika Kusini kuvaana na Marumo Gallants katika mchezo wa marudiano ambao unatarajiwa kupigwa Mei 17, mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kocha Riedoh alisema: “Marumo ni miongoni mwa timu zinazofanya vizuri ndani ya ligi ya Afrika Kusini. Licha ya kuwa ni timu changa sana lakini wamefanya uwekezaji mkubwa kuhakikisha wanakuwa na kikosi cha ushindani.
“Hii ni mara yao ya kwanza wanashiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika na unaweza kuona wamefanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali, hii inatosha kueleza ni kwa kiasi gani wana mipango mizuri. Ni kweli Yanga kwa sasa wanaonekana kuwa na kiwango bora lakini ni lazima wacheze kwa tahadhari kubwa michezo yote miwili kama wanataka kufuzu fainali.”