Kaburi la Maradona linavyotikisa Buenos Aires

 

Maradona

Wakati rafiki yake au tunaweza kumuita hasimu wake, Edson Arantes do Nascimento maarufu kama Pele akiwa amelala katika makaburi ya Ecumenical pale Santos, Sao Paulo, Brazil, yeye amelala katika makaburi ya Bella Vista pale Buenos Aires, Argentina. Namzungumzia Diego Armando Maradona.


Alifariki dunia jioni ya Novemba 25, 2020 katika Jiji la Buenos Aires. Ni baada ya kuambatana na matatizo mengi ya dunia ambayo hakuweza kuyahimili. Matatizo yaliyotokana na tabia zake binafsi pamoja na makuzi ambayo yalimpeleka kuwa supastaa mkubwa duniani.


Nadhani sura yake imeweka tabasamu akiwa amelala chini ya futi sita. Nadhani kaburi lake litakuwa linatikisika. Tena kwa furaha. Ingekuwa miezi sita ya ajabu kwa Maradona kama angekuwa hai. Naam miezi sita ya kustaajabisha.


Ndani ya miezi sita, Maradona angekuwa Doha, Qatar akishangilia Argentina ikitwaa Kombe la Dunia chini ya mtu anayehusudiwa kama yeye pale Argentina, Lionel Messi. Furaha iliyoje. Sijui Maradona angefanya vituko vya namna gani.


Angeingia uwanjani. Angemkumbatia Messi. Angemkumbatia Alex McAllister angemkumbatia Emiliano Martinez angemkumbatia kila shujaa wa Argentina. Na zaidi angeweza kufanya vituko ambavyo vingetuacha hoi wote ambao tulikuwa tunafuatilia pambano lile muhimu la pale Doha.


Siku za baadaye za maisha yake baada ya kufanya mambo makubwa katika soka Maradona aliathirika na dawa za kulevya.


Alikuwa mtu wa vituko, lakini aliendelea kuwa mwanadamu aliyeyafurahia maisha. Hata hivyo, zaidi ya kila kitu alilipenda taifa lake la Argentina.


Bahati mbaya hakupata nafasi ya kuliona taifa lake likitwaa Kombe la Dunia baada ya yeye na wenzake kufanya maajabu pale Mexico, 1986. Mungu hakumpa fursa hii. Alijaribu kama kocha pale Afrika Kusini 2010, lakini haikuwezekana. Alijaribu kama mshangiliaji wa kawaida lakini haikuwezekana.


Kama angekuwepo Doha usiku ule ambao Gonzalo Montiel alifunga penalti ya mwisho ya Argentina dhidi ya Ufaransa na kutwaa Kombe la Dunia nadhani Maradona angepandwa na kichaa. Nadhani wangemfunga kamba.


Nyumbani Argentina, Maradona alikuwa anawekwa mbele ya Messi kwa sababu alikuwa amechukua Kombe la Dunia. Hata hivyo, Maradona hakuwahi kuonea wivu uwezekano wa Messi kutwaa Kombe la Dunia.


Kwa raia wa Argentina haijawahi kuonekana kwamba Messi na Maradona wangeweza kuwekwa katika chungu kimoja kama Messi angetwaa Kombe la Dunia.


Kwao Maradona aliiendelea kubaki Maradona licha ya kuibuka kwa Messi. Wakati dunia nyingine ikiamini kwamba huenda Messi ni zaidi ya Maradona, lakini kwa Argentina wameendelea kuamini kwamba Maradona ni zaidi ya Messi.


Labda kwa sababu alitwaa Kombe la Dunia mapema. Labda kwa sababu wanashindwa kulinganisha zama. Kwao Maradona ni zaidi ya kila mchezaji yeyote yule. Hana mfanowe. Maradona hakuzuia Argentina isitwae Kombe la Dunia kwa sababu eti Messi angekuwa naye ametwaa kombe hilo. Jioni ile ya Doha angekuwa mwanadamu mwenye furaha duniani.


Kuongeza furaha isiyomithilika ya Maradona miezi mitano baadaye Napoli imetwaa ubingwa wa Italia juzi usiku. Kama Argentina ni taifa lake, basi Napoli ni timu ya maisha yake. Aliihifadhi Napoli katika moyo wake na mashabiki wakamhifadhi katika mioyo yao tangu siku ile aliyotua Napoli Julai 1984 na kisha akapokewa na mashabiki 75,000 katika dimba la San Paolo.


Ni Maradona ndiye aliyejaribu kubadili utawala wa soka la Italia. Wakati akifika hakuna timu kutoka upande wa Kusini ambayo ilikuwa imewahi kuchukua ubingwa wa Italia. Wakati huo mpira ulikuwa unatawaliwa na timu kutoka Kaskazini na kati. Maradona alizificha timu tawala kisha akaupeleka mpira Kusini mwa Italia ambapo alitwaa mataji mawili ya ubingwa wa Italia ‘Scudetto’ 1987 na 1990. Pale Napoli Maradona ni kama kufuru. Ni ‘mungu mtu’.


Na ndio maana haikushangaza uwanja wao ulipoitwa Uwanja wa Maradona wiki moja tangu alipofariki dunia 2020. Alifanya mambo makubwa katika mji wa kisela. Alihamia mji huo na ndugu zake kutoka Argentina.


Tangu 1990 kama ilivyokuwa kwa Argentina ambayo ni tangu 1986, Maradona alikuwa hajawahi kuiona Napoli ikichukua ubingwa.


Fikiria ndani ya miezi mitano tu angekuwa ameiona Argentina ikichukua Kombe la Dunia na kisha Napoli ikichukua ubingwa wa Italia. Angekuwa ameiona Napoli ikichukua ubingwa wa Italia baada ya miaka 33. Angepata wazimu. Angesafiri mpaka Napoli kwenda kushangilia ubingwa huu na wahuni wa Napoli. Napoli ni miongoni mwa timu zenye mashabiki wahuni barani Ulaya.


Haishangazi kuona walipatana vyema na mhuni mwenzao kutoka Argentina. Uwanjani Maradona alikuwa anaanzisha vurugu zake na anapata sapoti kutoka katika majukwaa. Nje ya uwanja alikuwa anakwenda kula nao unga. Haishangazi kuona matatizo mengi ya dawa za kulevya yalimkuta akiwa Italia na sio Hispania wala Argentina.


Kule Argentina, Maradona hadi wakati anafariki dunia hakuwa na matatizo na ubingwa. Alikuwa shabiki mkubwa wa Boca Junior na karibu kila msimu alikuwa akishuhudia ikitwaa ubingwa dhidi ya wapinzani wao River Plates ambao kuna wakati walifikia hatua ya kushuka daraja.


Kwa sasa, mmoja kati ya binadamu ambao wangepaswa kuwa na furaha zaidi duniani amelala pale Buenos Aires. Amepishana na furaha kubwa. Huwa inatokea. Vyovyote ilivyo ingekuwa miezi yenye furaha zaidi kwa Maradona. Mungu hakupenda itokee mbele ya uso wake. Alimtanguliza kabla ya kukiona ambacho wengine tumekiona. Tunaweza kufungua mvinyo na kusheherekea kwa niaba yake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.