HISIA ZANGU: Ally Salim alivyopoteza kila kitu ndani ya siku kumi

Published from Blogger Prime Android App

ZIMEKUWA takribani siku 14 za haraka kwa Mnyama Simba, lakini pia kwa kipa wao, Ally Salim. Wakati Enock Inonga na Kibu Dennis wakiiadhibu Yanga Aprili 16 pale Temeke, Simba walikuwa wakiingia uwanjani wakishiriki katika michuano mitatu.

Sio tu kwamba walikuwa wakishiriki, lakini itoshe kusema kwamba walikuwa wakishindana katika michuano yote. Na matazamio ni kwamba waangeweza kuondoka na kitu fulani katika michuano hii. Jioni hiyo walipunguza pengo lao na watani wao hadi pointi tano. Ubingwa ulionekana unawezekana.

Siku chache baadaye walikuwa wakiingia uwanjani kucheza na Wydad Casablanca. Wakashinda bao moja na ilikuwa inaonekana kwamba nusu fainali ni jambo linalowezekana. Siku chache baadaye wakapanda ndege kwenda Casablanca kucheza mechi ya marudiano mnamo Aprili 28.

Kuanzia Aprili 28 mpaka juzi Mei 7 kila kitu kimekwenda kasi na Simba hawapo katika mbio za michuano yoyote ile msimu huu. Kila kitu kimekwenda kasi. Simba imepoteza kila kitu na kuna shujaa mpya aliibuka katika pambano la Yanga, Ally Salim naye anaonekana amepoteza kila kitu.


Alidaka kama shujaa katika pambano la Yanga huku akiwa haaminiki. Hakuwa katika majaribio sana lakini uwezo wake wa kujiamini uliwakosha wengi, hasa mimi ambaye binafsi sikumuamini sana kama kipa.

Pambano muhimu la kwanza la kuwaweka Simba katika mashindano makubwa, Salim aliruhusu bao rahisi la Junior Sambou. Katika hatua kama hii haupaswi kuruhusu bao rahisi. Baadaye aliokoa mchomo mwingine wa Sambou lakini haikubadilisha ukweli kwamba alifungwa bao ambalo kama langoni kungekuwa na kipa mwenye uzoefu kama Aishi Manula basi angeucheza mpira ule.

Mwisho Simba walijikuta katika mikwaju ya penalti na wazoefu wawili, Shomari Kapombe na Clatous Chotta Chama wakakosa penalti zao. Salim hawezi kubeba lawama peke yake lakini kama angekuwa shujaa kama Juma Kaseja mwaka 2003 pale Cairo si ajabu wasingefika katika mikwaju ya penalti.


Simba walipotolewa katika michuano ya Afrika Aprili 28 wakajikuta wakiangukia katika pambano muhimu la Ligi Kuu dhidi ya Namungo Mei 3. Akili kubwa kwa kocha, Robertinho na mabosi wa timu nadhani ilikuwa kuelekeza nguvu katika michuano ya FA.

Haijulikani wazo lilikuwa la nani lakini Kapombe, Chama, Inonga, Mzamiru na Kanoute wakawekwa nje. Katika timu ambayo wachezaji wanaoanza na wale wanaokaa benchi kuna tofauti kubwa kati yao, Simba walitoka sare uwanja wa Majaliwa.

Bao la kusawazisha la Namungo kosa la nani? Huyu huyu Ally Salim. Mpira ambao angeweza kuupangua au kuudaka, aliugusa kidhaifu na mkono ukamuangukia Hassan Kabunda aliyefunga kwa urahisi. Bao la pili ndani ya siku tano ambalo liliwanyang’anya kitu muhimu.

Hili bao lilikuwa linamaanisha kwamba endapo Yanga wangemfunga Singida Big Stars kesho yake basi pengo baina yao lingekuwa pointi saba. Na ndicho ambacho kilitokea. Yanga alimfunga Singida ndani ya dakika za kwanza tu pale uwanja wa Liti na mpaka sasa anahitaji ushindi mmoja katika mechi mechi tatu awe bingwa.


Baada ya hapo Simba wakafunga safari ya kwenda zao Mtwara katika pambano ambalo nadhani walilihitaji kuliko pambano lolote msimu huu kwa mujibu wa hesabu zao za msimu zilivyokwenda. Mapumziko ya akina Chama ilionekana kama vile yangelipa msimu huu.

Hata hivyo, alikuwa ni Ally Salim aliyeanza kuwaangusha mapema kama ilivyo kawaida yake, mpira wa adhabu ambao ulikuwa unaonekana kwenda katika mikono yake akaurudisha kwa kifua na Azam wakapata bao la kuongoza.

Simba walirudi mchezoni baada ya Sadio Kanoute kusawazisha lakini Salim akafungwa tena bao rahisi na Prince Dube katika kipindi cha pili. kama Salim angetulia langoni alikuwa anaudaka vizuri tu mpira wa Dube lakini yeye akatoka langoni wakati Josh Onyango akiwa hajamalizana na Dube.

Mwisho wa mchezo Simba ikiwa imepoteza kila kitu. sioni tena kama wanaweza kuukwapua ubingwa katika mikono ya Yanga. Pointi saba ni nyingi. Wametupwa katika ligi ya mabingwa na wametupwa nje katika michuano ya Shirikisho. Wanaondoka bila ya taji lolote kwa mwaka mwingine tena.


Kwanini? Hawana tena timu kubwa kama waliyokuwa nayo ile wakati ule wakiwa na machaguo mengi kila eneo. Hawa tena timu yenye kariba ya Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Rally Bwalya, Chama, Louis Miquissone, Meddie Kagere, John Bocco, Chris Mugalu na wengineo. Mpira ni mchezo wa hadharani.

Hapa katikati wamekosea mara nyingi katika madirisha ya uhamisho ya wachezaji. Bado timu yao haijavunjika sana na wanaweza kuirudisha haraka katika reli endapo wataletwa wachezaji ambao watakuja kutoa upinzani mkubwa katika kikosi kinachoanza.

Katika mpira wa kisasa timu haipaswi kuwa na kikosi imara cha kwanza kinachoanza tu. Timu inapaswa kuundwa na kundi la wachezaji 25 ambao wote wana uwezo mkubwa wa kuanza mechi bila ya kuhoji. Hata wapinzani wao Yanga, kuna wachezaji wawili tu ambao unatabiri lazima wataanza mechi. Djigui Diarra na Fiston Mayele wengine wote wanaweza kuanza mechi na ukawaamini.

Simba wanaweza kurudi imara na kuchukua wachezaji wa maana katika maeneo muhimu hasa eneo la kiungo ambapo kama Kanoute na Mzamiru hawachezi basi inakuwa shida tupu. Unaporuhusu Azam wawe na mchezaji kama James Akaminko na wewe unabakiwa na Ismail Sawadogo tatizo linaanzia hapo.

Kwa upande wa Salim pia nadhani amepoteza nafasi ya kuibuka kuwa mmoja kati ya makipa hodari nchini. Kama angekuwa hodari basi hii ilikuwa nafasi yake ya dhahabu. Makipa wengi wa kwanza wametokana na matatizo ambayo yamewatokea makipa wakubwa ndani ya timu.


Huku ikionekana kuwa Beno Kakolanya anaelekea Singida Big Stars ni wazi kwamba yeye angekuwa kipa wa pili nyuma ya Aishi Manula kama angefanya vema. Na inawezekana pia kama angefanya maajabu basi angeweza kuwa kipa namba moja kabisa kwa sababu kuna wakati kumekuwa na misuguano ya chini chini ya Simba na Aishi.

Tazama kile ambacho kinda, Clement Mzize amefanya Yanga ametoka kusikojulikana lakini ameitumia vema nafasi yake. Hii ndio namna ambayo Salim alipaswa kuitendea haki nafasi yake lakini ninachokiona kwa sasa Simba wataingia sokoni kusaka kipa mwingine mahiri kwa ajili ya kuja kuchuana na Aishi.

Hata kama haitakuwa nje ya nchi lakini kuna makipa wengi ndani ya nchi ambao wanaweza kustahili kuwa makipa wa pili Simba kuliko Salim. Hili ni tatizo lingine ambalo Simba inabidi walifanyie kazi kwa umakini.

Kifupi mashabiki wa Simba wanawatazama viongozi wao kujua nini watafanya katika dirisha kubwa lijalo la uhamisho. Kwa kilichowatokea kwa msimu wa pili mfululizo litakuwa dirisha linaloleta hamu kwa mashabiki wa Simba. Viongozi wasiwaangushe. Wakiwaangusha tena kwa mara ya tatu nadhani hakutakalika vema. Mashabiki wanaficha makucha yao kwa sababu timu iliwapa furaha miezi 24 iliyopita. Baadaye huwa wanachoka. Wakichoka huwa hawaendi uwanjani wala kununua jezi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.