Ahmed Ally |
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Kalbu ya Simba, Ahmed Ally amesema kuwa uongozi wa klabu hiyo na idara zote zitafanya tathmini kwa wachezaji wote, benchi la ufundi na watendaji wote wa timu baada ya kukosa taji hata moja msimu mzima.
Ahmed amesema hayo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Azam FC, mkoani Mtwara ambapo Azam waliibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Simba na kufanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo.
“Sisi kama Simba lazima tuangalie tunakosa wapi, kwa miaka miwili tunaishia palepale, msimu uliopita mashindano ya CAF tuliishia robo fainali, Kombe la Shirikisho la Azam tukaishia Nusu Fainali (kufungwa na Yanga) na Kombe la Ligi Kuu nafasi ya pili, na msimu huu ni hivyo hivyo.
“Tafsiri yake ni kwamba klabu yetu haija piga hatua, maana yake lazima turejee kwenye maabara yetu kuna shida sehemu gani. Tutazame je, aina ya wachezaji tulio nao wanaweza kutusaidia kuchukua ubingwa?
“Tufanye tathmini ya mchezi mmoja mmoja. Huyu mchezaji atatusaidia kwenda mbele au kubaki palepale? Lazima tufanye tathmini ya benchi la ufundi, watu tulio nao watatusaidia kupata mataji tunayoyataka?
“Huu ni ukweli kwamba kama miaka miwili tunaishia palepale, maana yake watu ulionao hawana uwezo wa kukutoa pale ulipo kukupeleka hatua ya mbele zaidi. “Yawezekana walikuwa bora nyakati hizo, wakafanya vizuri wakati huo, lakini sasa wana huo ubora wa kututoa hapa kwenda hatua nyingine? Na wale ambao tuliwaleta kutusaidia kutoka hapa kwenda hatua nyingine, wana huo ubora wa kutusaidia kuchukua mataji?” Amesema Ahmed.
Baada ya tathmini hiyo kukamilika kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya nyita wa timu hiyo wakaachana na klabu hiyo ili kutoa fursa kwa klabu kufanya usajili na kuboresha kikosi chao ili waweze kufikia malengo yao waliyojiwekea.
Mpaka sasa unaweza kusema Simba imekosa mataji yote msimu huu, kwani wametolewa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye hatua ya robo fainali, Kombe la Shirikisho la Azam wametolewa, ngao ya jamii wamekosa, Mapinduzi Cup wamekosa n ahata ubingwa wa Ligi, Yanga ndiyo inaonongoza huku ikihitaji mchezo mmoja tu kutangaza ubingwa kati ya mitatu iliyosalia kutamatika kwa ligi.